30 Sep 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kashkash za vijana wa Tibaigana Dar
 
2005-09-30 17:57:26
Na Mwandishi wetu , Jijini

  Bw. Tibaigana  
   
Mitaa ya Ohio na Sokoine jana ilionekana kama uwanja wa vita au eneo la kutengenezea filamu za aksheni wakati vijana wa Tibaigana walipovamia eneo hilo jana katikapurukushani ya kukabiliana na majambazi.

Hata hivyo vijana hao walimtia mbaroni mwanamke mmoja ambaye ana kesi lukuki za kitapeli. Miondoko ya Landrover zaidi ya tatu kuingia katika benki ya Baroda kuliashiria shari katika eneo hilo maarufu kwa mabenki na mashirika yenye kujinafasi.

Wananchi wa Dar kama kawaida wasivyojua hatari mara moja walinusa hasira za wapiganaji hao na kukimbilia eneo hilo huku wakiwa hawajui kwamba wanaingia eneo la operesheni.

Vijana hao wengine wakiingia kupitia Ohio na wengine Sokoine, walikuwa wakidondoka mmoja baada ya mwingine katika magari yaliyokuwa yakienda kasi huku yamewasha mijitaa ya hatari.

Wakati gari zinafunga breki magari hayo yalikuwa hayana watu zaidi ya madereva na kama filamu walitumbukia katika jengo la benki hiyo ambayo zamani lilikuwa ni jengo la kasino.

Kwa staili ya kuingia katika eneo hilo, majambazi inabidi nayo yajifunze njama mpya kwani inaonekana askari hao walikuwa katika hadhari kubwa lakini wakiwa na kasi.

Katika siku za karibuni kumekuwepo na mawindo makali ya majambazi kufuatia vurumai zao zilizowapagawisha wakazi wa Dar es salaam.

Mara baada ya kujitoma ndani askari haow alitoka na mtu wao wakiwa wanamkwida kijabari kabisa kumtupa katika gari na kuanza kumpa kisago papo hapo.

Ilionekana dhahiri kwamba askari hao walikosa ile shamrashamra inayoambatana na miluzi ya risasi kwa jinsi walivyomshughulikia mama huyo ambaye kwa umbile alikuwa anaonekana mtu wa mikashikashi.

mashuhuda wa matukio hayo tangu yanaanza walisema ilikuw a taabu sana kutoka kwenda eneo jingine kwa jinsi wanaume wa TZR walivyokuwa wakitamba eneo hilo.

Maeneo hayo ya mabenki ya CRDB (Holland House), Eurafrika,Stanbic na Standard ni eneo lenye shughuli nyingi sana na pilikapilika kubwa.

Kamanda wa polisi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba vikosi vitatu vya polisi wa kukabiliana na ujambazi viliingia eneo hilo kutokea pande tofauti baada ya kuwataarifu kuwa kuna ujambazi benki hiyo.

Alisema Bw. Tibaigana kuwa alipata taarifa za kuwepo kwa ujambazi unaokusudiwa kufanyika kwa hiyo aliwaagiza vijana wake ambao wako mitaani kukabiliana na uhalifu kwenda hapo mara moja.

’’Ahh lakini tulimkamata mwanamke huyu tapeli,’’ alisema. Mwanamke huyo anadaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya kitapeli alikuwa katika jaribio la kuiba Sh. milioni 6 kwa kutumia hundi feki katika benki hiyo ya Baroda.
Katika jaribio hilo mwanaume aliyeongozana naye aliingia mitini baada ya kugundua kuwa njama yao imebainika.

Tukio hilo lilitokea saa saba mchana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dar es Saalam, Bw. Alfred Tibaigana.

Kamanda Tibaigana alisema mwanamke huyo akiwa ameongozana na mwanaume huyo, walikwenda kwenye benki hiyo wakiwa na hundi feki ya Sh. milioni 6 inayoonyesha imetoka kwenye akaunti ya hospitali ya Tumaini, ya jijini Dar es Salaam.

Alisema akiwa ofisini kwake alipokea simu kutoka kwenye benki hiyo ikimtaarifu kuwa kuna majambazi wameingia kwenye benki hiyo wakitaka kuiba.

’’Nilipokea simu ikiniarifu kuna majambazi wanataka kuiba kwenye benki hiyo, ndipo nilipotuma vikosi vya askari vikiwa na magari yao ili kupambana na majambazi hayo na kufanikiwa kumtia nguvuni mwanamke huyo na mwezake alishtuka na kukimbia’’, alisema Kamanda Tibaigana.

Alisema kwa mujibu wa maelezo ya Mhasibu aliyepokea hundi hiyo, kutoka kwa tapeli huyo, aliitilia shaka kwa kuwa wanaokuja kuchukua fedha za hospitali hiyo anawafahamu.

Alisema mara baada ya kutilia shaka, Mhasibu huyo alipiga simu polisi na ndipo mwanamke huyo akakamatwa akiwa bado hajatoka nje ya benki.

Kamanda Tibaigana alisema, vielelezo vya polisi vinaonyesha kuwa mwanamke huyo anahusika kwenye matukio mbalimbali ya utapeli jijini na kuwa ana kesi zaidi ya nne mahakamani.

’’Mwamamke huyo ni tapeli wa siku nyingi tena maarufu hivi sasa ana kesi kama nne mahakamani, ila kwa muda huo aliofanya tukio hili alikuwa nje kwa dhamana,’’alisema Bw. Tibaigana.

Kamanda Tibaigana alisema katika kesi zilizopo mahakamani , mwanamke huyo anatuhumiwa kwa kujifanya mwalimu wa shule kisha kugushi vyeti na kuchukua mikopo kwenye benki ya NMB.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.