|
Mmoja agongwa na gari na kufa wakati akivuka barabara
2006-04-22 15:30:07
Na Mwanaidi Swedi, Polisi
Mkazi mmoja Bw.Sailep Kamuja, 28, amekufa baada ya kugongwa na gari wakati anajaribu kuvuka barabara.
Ajali hiyo imetokea pale Njiapanda Kunduchi Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamishna Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana tukio hilo lilitokea jana saa 6:00 mchana huko eneo la Njiapanda ya Kunduchi.
Amesema mtu huyo aligongwa na gari lenye namba za usajili T459 AFE aina ya Toyota Land Cruser iliyokuwa likiendeshwa na dereva Immanuel John,36, kutokea Mbweni kuelekea Tegeta.
Aidha amesema dereva aliyesababisha kifo hicho anashikiliwa na polisi wakati mwili wa marehemui umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakati huohuo, watu 19 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukamatwa na bangi misokoto 25 pamoja na kete 40 za madawa ya kulevya katika maeneo tofauti Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Tibaigana amesema tukio la kwanza lilitokea jana kati ya saa 4:00 na saa 7:00 mchana huko kwenye barabara ya Kawawa eneo la Shaaban Robert karibu na umoja House Jijini Dar es Salaam ambapo polisi iliwakamata watu 7 wakiwa na bangi misokoto 25.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ally Fadhili, 21, Kelvin Mgaya 18, Mwinyi Athuman 19,Fikira Charles 18, na Musa Miser 15.
Wengine ni Lazaro Juma,14, Festo Erinest 17, Moshi Idd 16, Amemu Tomasi 22 Saisi Zakaria, 17.
Katika tukio jingine, Polisi Jijini wanawashikiliwa watu 12 ambao walikamatwa kati ya saa 6:00 na saa 12:00 jioni huko Gongolamboto na Mwenge.
Amesema katika tukio hilo askari walifanya msako na kuwakamata watu 7 wakiwa na kete 40 za madawa ya kulevya.
Akasema pia waliwakamata watuhumiwa watano wakiwa na bangi misokoto 5 pamoja na gongo lita kadhaa.
|