22 Apr 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watumishi wa umma wazembe kung’oka
 
2006-04-22 15:31:53
Na Lulu George,Tanga

Serikali imesema itawachukulia hatua kali watumishi wa umma watakaoshindwa kutimiza wajibu wao kwa kwenda kinyume na maadili ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kazini mara moja.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bi. Hawa Ghasia (MB) wakati akifungua mkutano wa kwanza kwa watumishi wa umma tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya nne uliofanyika katika hoteli ya Mkonge mjini hapa.

Amesema ni ukweli usiopingika kuwa katika utumishi wa umma kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili na kwamba baadhi ya watumishi wanatenda mambo ambayo ni kinyume na sera,sheria kanuni na miongozo ya taaluma zao.

Amesema hayo yanatokea kwa sababu watumishi wa umma wanatumia nafasi walizonazo kwa maslahi yao binafsi,hivyo serikali haina budi kukemea na kupiga vita tabia hizo mbaya na ninazochangia kiuipaka idara hiyo matope.

Ameongeza kuwa sekta ya utumishi wa umma bado inakabiliwa na tatizo la kuzorota katika utendaji kazi, hali inayosababishwa na watendaji wakuu katika wizara, idara za serikali zinazojitegemea na sekretarieti za mikoa kutojua wajibu wa kazi zao.

’Viongozi wakuu katika idara hii wana uoga pamoja na uzembe kwa kutofanya kazi walizoteuliwa kuzifanya...hii ni tabia chafu na mbaya sana ambayo Serikali haitaweza kuvumulia...tutawang’oa tu,’akasisitiza Waziri.

Hata hivyo ametoa wito kwa viongozi hao kutekeleza majukumu wanayopewa na Serikali kwa ustadi, haraka na kwa ufanisi sambamba kuwa waadilifu na wenye kuwajibika kwa dhati katika kutoa huduma bora kwa umma .

Alisema Serikali ili iweze kuaminika, lazima iwe na watumishi wa umma ambao ni wachapakazi ,wanaosikiliza shida za wananchi pamoja na kuwa na ari katika shughuli za utawala ikiwa pamoja na kusimamia, kuongoza pamoja na kutekeleza misingi ya sera, sheria na kanuni za kazi.

Mkutano huo wa kwanza kwa mwaka 2006 wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma unawashirikisha wakurugenzi wa utawala na utumishi, maafisa tawala na watumishi wakuu wafawidhi katika Idara za Serikali zinazojitegemea pamoja na makatibu tawala wasaidizi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.