|
Benki ya NMB kuhudumia waliojeruhiwa
2006-04-22 15:41:23
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Benki ya NMB imeahidi kuwahudumia watu waliojeruhiwa kwenye sakata la ujambazi lililotokea juzi pale kwenye mataa ya Ubungo.
Uongozi wa benki hiyo umetoa msimamo huo ulipokwenda kuwatembelea majeruhi hao waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili, MOI.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Bw. Meshack Ngatunga ameliambia gazeti hili kuwa ni wajibu wa benki hiyo kuwahudumia kwa kutoa gharama za matibabu kwa majeruhi hao.
Bw. Ngatunga hata hivyo hakuwa tayari kueleza juu ya watu waliouawa kama benki hiyo itatoa msaada kwa familia zilizofiwa.
Ni mapema kusema hilo. Kinachosubiriwa ni hatua ya polisi kufanya uchungzi wao, alisema Bw. Ngatunga.
Watu waliokufa katika tukio hilo wametambuliwa kuwa ni PC Abdallah na mtumishi wa Benki hiyo Bw. Evarist Manyoni.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa shukurani kwa Jeshi la Polisi nchini hasa kwa askari mmoja aliyejitoa mhanga kupambana uso kwa uso na majambazi hayo hadi kuokoa kiasi cha Sh. Milioni 850 kati ya Sh. Bilioni moja ambazo zilikuwa zikisafirishwa.
Akiongea na gazeti hili, Polisi aliyejeruhiwa, Adim Kilomoko alisema anajisikia maumivu makali sehemu ya mguu wake ambao ulivunjwa na risasi za majambazi hayo.
Pia risasi nyingine ilimpata sehemu ya kichwani.
Hata hivyo madaktari wamesema risasi hiyo haiwezi kuhatarisha maisha yake kwa kuwa haijapenya hadi katika kiwambo cha fuvu la kichwa.
Najisikia bado maumivu makali sehemu ya mguu, sina maumivu mengine zaidi ya hayo nawashukuru madaktari wakati wote wamekuwa macho kunihudumia, akasema Bw. Kilomoko.
Kaimu Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Frank Matua amesema afya ya polisi huyo pamoja na majeruhi mwingine Mzee Ali Mohamed, 60, inaonyesha kuimarika kutokana na matibabu wanayopewa na madaktari katika wodi namba 17 ambako wamelazwa.
|