|
Ushirikina kibao Messina, Baghdad
2006-07-10 14:24:12
By Majuto Omary, Urafiki
Mechi ya soka iliyochezwa uwanja wa Urafiki kuwania sh. milioni 1 za michuano ya kombe la Kinesi kati ya Messina na Baghdad zote za Magomeni, imetawaliwa na imani za kishirikina.
Kabla ya mechi hiyo kuanza, kila timu ilionekana kujiandaa na kamati ya ufundi ya kienyeji na kuwafanya watazamaji waliokuwa nje kuanza kuogopa pamoja kutokana na kutokuwa miongoni mwa wachezaji.
Makaratasi yaliyoandikwa maandishi ya kiarabu yalizagaa uwanjani hapo huku moja likiwekwa kwenye benchi la mwamuzi wa akiba wa mchezo huo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha soka cha Manispaa ya Kinondoni, KIFA, Frank Mchaki alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema kuwa wao wamejitahidi kwa kadri ya uwezo wao kukemia vitendo hivyo, lakini timu bado zinaendekeza.
Mchaki amesema hata katika ligi ya wanawake kuna vitendo vya kiushirikina na KIFA imeandaa adhabu kali kwa timu ambazo zitabainika kufanya mambo hayo.
Siyo mechi hii tu hata ligi ya wanawake kuna mambo haya, sasa tunaweka utaratibu wa adhabu ili kuondoa haya, mpira hauchezwi kwa ushirikina na viongozi wanatakiwa kubadilika, amesema Mchaki.
Mechi hiyo iliyoisha kwa Messina kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, imechezeshwa na mwamuzi Saltin Sanga na mbali ya imani hizo potofu, pia imetawaliwa na upinzani mkubwa wa jadi kuanzia kwa wapenzi na wachezaji.
|