|
Mayay,Nyanda waiongoza Abajalo
2006-07-11 14:55:38
By Hussein Omar, Urafiki
Abajalo FC Mnyama Mkubwa\ ya Sinza, ikiongozwa na wachezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay na Aron Nyanda, juzi wamefanikiwa kuwafunika Sinza Stars kwa kuwafunga mabao 3-1 katika mchezo wa kuwania kombe la Kinesi.
Mchezo huo uliochezwa uwanja wa Urafiki, Jijini, ulikuwa na upinzani mkali kutokana na timu hizo kutambiana kwa muda mrefu.
Mayay alianza kufumania lango la Sinza dakika 12 kipindi cha kwanza baada ya kuihadaa ngome ya wapinzani wake na kupiga shuti kali.
Kama haitoshi Abajalo wakapata bao la pili dakika 14 kupitia kwa Jeremiah Mboma mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Vijana walio chini ya miaka 17.
Baada ya mabao hayo, Sinza Stars wakafanya mabadiliko kwa kuwaingiza Kelvin na Denis Goliama.
Abajalo wakazidi kuonyesha umaarufu wao katika soka, baada ya kupachika bao la tatu dakika ya 32 kupitia kwa Mboma baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mayay.
Kipindi cha pili, Abajalo wakawaingiza Nyanda na Robert Kalikawe ambao hata hivyo hawajabadilisha matokeo tena.
Bao pekee la Sinza lilipachikwa na Hamis Bamba katika dakika ya 75 ya mchezo.
|