|
Manyema yasuswa na waamuzi wa TMK
2006-07-11 14:57:21
By Mariam Mkumbaru, Tandika
Baada ya mashabiki wa timu ya soka ya Manyema ya Jijini, kuwadunda mara kwa mara waamuzi, Cham cha Waamuzi Manispaa Temeke, kimeamua kuisusa timu hiyo katika michezo yake.
Maamuzi hayo yametolewa na chama hicho, FRAT- Temeke baada ya timu hiyo kuwafanyia vurugu baadhi ya waamuzi waliochezesha mechi ya kirafiki kati ya Likwati na Manyema.
\Hatutaichezesha tena Manyema ya Ilala, kwani imezoea kutufanyia fujo huku viongozi wake wakiwa mstari wa mbele kushabikia bila ya kuonya wachezaji ama mashabiki wao,\ amesema mwamuzi Simba Mwaisame.
Vurugu hizo za juzi, zilianza baada ya mchezaji wa Manyema, Daudi Paulo, kupewa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji wa Likwati, Yusuph Fundi dakika ya 62 hali iliyosababisha wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kufanya vurugu.
Mwamuzi wa mchezo huo baada ya kutoa kadi hiyo nyekundu, akavamiwa na kunusurika kupigwa huku akitukanwa matusi mazito mazito ya nguoni.
Naye kiongozi wa Likwati, Alex Mulisa amesema amesikitishwa na tukio hilo kwa viongozi wa Manyema kuwa mstari wa mbele kuchochea vurugu hizo pamoja na kuitoa timu uwanjani baada ya imezidiwa.
Hiyo ni mara ya tatu kwa timu hiyo ya Kariakoo kuwafanyia vurugu waamuzi wa Temeke, baada ya awali kufanya hivyo ilipocheza na Sacramento pamoja na Temeke Squad.
|