|
Wapiga debe kero tupu vituoni-UMMAWADAR
2006-08-28 17:31:16
Na Francisca Jeremiah
Chama cha Umoja wa Madereva, Makondakta na Wasimamizi wa foleni katika vituo wa mabasi ya daladala Jijini, UMMAWADAR,wameiomba Serikali kuendesha tena zoezi la kuwaondoa wapiga debe vituoni.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Juma Mburu wakati akiongea na gazeti hili ofisini kwake, Jijini.
Amesema mikakati ya chama hicho ni kuimarisha usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwangoa wapiga debe hao kwa kuwa wamekuwa kero kwa abiria, madereva na makondakta wenyewe kwa kuwatishia maisha.
Serikali isihangaike na majambazi tu bali pia iwafagie wapiga debe ambao ni kero kubwa kwa abiria, madereva na makonda,akadai Bw. Mburu.
Aidha amesema kuwa kwa sasa chama hicho kimeshaanza kufanya kazi yake ya kuwaondoa wapiga debe katika baadhi ya vituo vya daladala.
Amevitaja vituo hivyo kuwa ni pamoja na Tandika kupitia Changombe na shule ya Uhuru ambapo mpaka sasa hali ya usalama ni nzuri na magari yanafuata utaratibu.
Amesema chama hicho kimeshaanza kuwaendeleza madereva wao kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yahusianayo na kazi yao kwa kuwapeleka vyuoni.
Amesema mpaka sasa madereva 30 wameshafuzu masomo hayo.
Vilevile uongozi wa chama hicho umeomba Serikali kuwasaidia juu ya upatikanaji wa ajira kwa madereva na makondakta kwa kuweka sheria zitakazowabana wamiliki wa magari kuwapa ajira ya kudumu.
Uongozi huo umesema idadi kubwa ya madereva na makondakta wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na kukosa ajira.
Wamiliki wanachojali ni mahesabu yao yatimie wala hawamjali dereva anayekamilisha mahesabu hayo, akasema Mwenyekiti huyo.
Aidha wamewataka madereva kujiunga na chama hicho ili maslahi yao yalindwe.
|