|
Mtoto toka Kenya abeba Mil. moja mashindano ya kuhifadhi Koran
2006-10-17 14:54:51
Na Haji Mbaruku, Jijini
Kijana mdogo mwenye umri wa miaka 15 ambaye pia ni raia wa nchini Kenya, Abdul Wahid Mohamed Yussuph, amejinyakulia zawadi ya shilingi milioni moja baada ya jopo la majaji kumchagua kuwa mshindi wa mashindano ya kuhifadhi Koran yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mashindano hayo yalikuwa yakihusisha wasomaji mbalimbali toka Afrika Mashariki wenye uwezo wa kuhifadhi Koran.
Katika mashindano hayo ambayo mgeni wake wa heshima alikuwa Makamu wa Rais, Dk.Ally Mohamed Shein, kijana Abdul aliwashinda wasomaji wenzake katika uhifadhi wa juzuu 30 za Koran.
Washindi wengine walikuwa Ally Abdallah Said, 11, na Madina Hamad, 7 wote wakazi wa hapa Jijini, katika mashindano ambayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa waumini wa dini ya Kiislamu.
Kijana Abdul alionekana tangu mwanzo kuwa angeshinda zawadi hiyo kutokana na umahiri mkubwa wa kusoma Koran aliouonyesha kwa majaji mbalimbali wa mashindano hayo.
Pia, mashindano hayo yalihudhuriwa na Rais mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Hamad Al Mazrui, Waziri Kiongozi mstaafu, Dk.Gharib Bilal na Dk.Hussein Mwinyi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Muungano.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi, makamu wa Rais, Dk.Shein aliitaka jamii iwe makini hasa katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wamepotoka kimaadili.
Amesema kuwa, waumini wengi wamebaki majina tu lakini hawana imani yoyote juu ya mola wao.
Aliwapongeza pia waandaaji wa mashindano hayo, Tanzania Muslim Hajj Trust na Madrasatul Fatahil Islamiya kwa kuwaleta wasomaji wa Koran akisema kuwa hatua hiyo inajenga umoja miongoni mwa waumini wa dini hiyo.
|