17 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kitimtim Mchikichini leo
 
2006-10-17 15:02:36
Na Emmanuel Lengwa, Mchikichini

Kitimtim cha aina yake kimetimka leo asubuhi kwenye maeneo ya soko la Mchikichini baada ya mgamo wa Jiji zaidi ya 50, askari polisi kuwazukia Machinga.

Machinga waliokumbwa na kimbembe hicho ni wale wanaofanya biashara nyuma ya kituo cha mabasi ya daladala cha Karume katika barabara ya Uhuru.

Katika kitimtim hicho kisichokuwa cha kawaida, mali kadhaa za Wamachinga waliokuwa wamekaidi kulihama eneo hilo zimetiwa moto na mgambo wa Jiji, huku Machinga zaidi ya 10 wakizolewa kwenye ’deffender’ mbili za polisi zilizokuwa zikishiriki operesheni hiyo kali na ya aina yake iliyowahusisha pia askari wa kutuliza ghasia, FFU.

Pia mibomu kadhaa ya machozi ilimwagwa eneo hilo, ikiwa ni katika harakati za kuwatimua Wamachinga waliokuwa wakijibu mapigo ya kuchomwa moto kwa mali zao wakitumia mawe na kuzomea vikosi vilivyokuwa vikishirikiana kuwadhibiti.

Katika zoezi hilo lililochukua saa kadhaa asubuhi leo, mabanda kibao yamesambaratishwa huku mali za wamachinga vikiwemo nguo, viatu, mabegi na vitu vingine walivyokuwa wakiuza vilikusanywa na kuonekana vikimwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto na mgambo wa Jiji.

Alasiri ilitinga eneo la tukio na kujionea hali halisi ambapo lilishuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiondoa mali zao na wengine kushindwa kuhamisha na hivyo kukumbwa na hasara ya kuteketezwa kwa mali zao.

Baadhi ya wafanyabiashara walisikika wakilalamika kuwa wametiwa hasara ya mwaka na hivyo hawajui watalipaje mikopo ya biashara hizo.

Wafanyabiashara hao wanadaiwa kufanyia shughuli zao eneo lisiloruhusiwa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wafanyabiashara wote walihamishiwa kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao na kuondolewa maeneo yasiyoruhusiwa.

Maeneo waliyotengewa Wamachinga ni Mbagala Zakhem, Sterio na Redio Tanzania wilayani Temeke, Mchikichini, Kilwa na Kigogo Sambusa wilayani Ilala na Mburahati, Urafiki, Mbezi Luis, Makumbusho, Kawe na Tegeta wilayani Kinondoni.

Miaka ya hivi karibuni kulikuwa na operesheni ya kuwaondoa wamachinga ambapo mgambo mmoja alifariki katika vurumai hizo.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye wafanyabiashara hao walirejea katika maeneo hayo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.