|
Majambazi yaua kwa risasi, yaambulia Sh.5, 000
2006-10-18 18:09:04
Na Usu-Emma Sindila, Temeke
Majambazi yenye roho ya kinyama na yaliyo tayari kufanya lolote alimradi kutimiza malengo yake yameua mtu kwa kumpiga risasi ya kichwa, kujeruhi wengine wawili kwa silaha hiyo.
Hata hivyo licha ya kufanya unyama wote huo, yameula wa chuya kwa kuambulia Sh. 5,000 za Kibongo badala ya mamilioni waliyotarajia.
Tukio hilo la kusikitisha limejiri pale Mbagala Kichemchem, jijini Dar es Salaam, ambako majambazi hayo yaliyokuwa matano, huku yakitumia bunduki, marungu na mapanga, kuvamia nyumba inayomilikiwa na Mhasibu wa Wizara ya Miundombinu Bw. Joachim Ndibalema na kufanya kufuru hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke Bw. Emmanuel Kandihabi, amedhibitisha tukio hilo na kuiambia Alasiri kuwa mmiliki wa nyumba hiyo, amejeruhiwa kwa risasi zilizofyatuliwa begani kwake huku mdogo wake Bw. Gideon Ndibalema, akipoteza maisha baada ya risasi hizo kulengwa kichwani mwake.
Mwingine aliyejeruhiwa vibaya katika tukio hilo lililojiri mishale ya saa 2:00 usiku ni mwanafamilia aliyetambulika kwa jina la Zuwena Dotto Abdul.
Yeye amekuwa hoi baada ya kupigwa marungu kadhaa mwilini mwake.
Taarifa zaidi za majirani zimesema kuwa majambazi hayo yalivamia nyumba hiyo wakati wenye nyumba wakijiandaa kupata mlo wa usiku.
Imeelezwa kuwa ghafla, wenyenyumba walisikia geti la nyumba yao likigongwa na walipouliza ni nani, aliyekuwa akigonga alisema ana mzigo wa mama na hivyo kufunguliwa kirahisi.
Zikasema taarifa hizo za watu wa karibu na wahanga wa tukio hilo kuwa baada ya mtu huyo kukabidhi huo mzigo usiotajwa, majambazi wakajitoma ndani, ikiwa ni baada ya kumuua palepale mlangoni kwa risasi ya kichwa kijana Gideon Ndibalema aliyewafungulia geti hilo.
Kuhusiana na mali zilizoporwa baada ya kufanyika kwa tukio hilo, Kamanda Kandihabi amesema: Licha ya kuua na kujeruhi, yameambulia simu moja ya mkononi na fedha taslim kiasi cha sh. 5,000... kisha yakaondoka. Hadi sasa, hakuna aliyekamatwa na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.
|