|
Machinga walipuka
2006-10-18 18:11:08
Na Usu-Emma Sindila, Temeke
Askari mgambo watano wa Manispaa ya Temeke wamejeruhiwa katika vurugu kali zilizolipuka jana kati ya wafanya biashara ndogo ndogo maarufu kama Machinga na askari hao.
Patashika hilo lilizuka katika soko la Tandika jana saa tano asubuhi.
Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Kamanda wa Polisi Temeke, Emmanuel Kandihabi amesema katika tukio hilo, mgambo watano walijeruhiwa na watatu kati ya hao, wamelazwa katika hospitali ya Temeke.
Walioshuhudia wanasema vurugu hizo zilitokea baada ya mgambo waliokuwa katika doria ya kila siku kuhakikisha maeneo ya wazi hayavamiwi na taratibu zote za kufanya biashara zinafuatwa, kuvamiwa na kundi la Wamachinga wenye hasira kali na kuanza kuwarushia mawe.
Kwa mujibu wa Kamanda Kandihabi, Wamachinga 41 walitiwa mbaroni na 19 kati yao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Amesema mgambo hao walikuwa katika doria na walipofika eneo hilo ambalo Wamachinga hawaruhusiwi kufanyia shughuli zao, wakavamiwa na kuanza kupigwa kwa mawe.
Amesema mgambo hao walipata msaada toka kwa askari polisi ambapo walifanikiwa kuwatia mbaroni baadhi ya Wamachinga waliokuwa mstari wa mbele katika vurugu hizo.
Amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Rehema Mwakiponda aliyejeruhiwa sehemu za kichwa na kisogoni, Ibrahimu Mwakani,45, sehemu za nyonga ya kulia na Rashid Mhina,45, aliyejeruhiwa mguu wa kulia na wote wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Temeke.
Amewataja wengine waliojeruhia kuwa ni Mwanahamisi Khalfan,32 aliyejeruhiwa sehemu za kifuani na Saka Joseph, 24 aliyejeruhiwa mguu wa kulia.
Jana hiyo hiyo Machinga wanaofanyia shughuli zao karibu na soko la Mchikichini pale Karume, walikurupushwa na bidhaa zao kutiwa moto.
Katika tukio hilo, Machinga kumi walitiwa mbaroni.
|