19 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kanisa ’lamwaga’ misaada ya viti vya walemavu
 
2006-10-19 20:40:09
Na Kiyao Hoza, Jijini

Licha ya kutoa huduma za kiroho kwa waumini wake, kanisa la Christian Mission Fellowship linatarajia kumwaga msaada wa viti 550 vya kutembelea kwa watu wenye ulemavu nchini.

Msaada huo ni miongoni mwa jitihada za kanisa hilo kuisaidia serikali katika kuwaondolea kero wananchi wake, hasa wa jamii hiyo ya walemavu.

Askofu wa kanisa hilo Bw. Mgullu Kilimba, ametoa ahadi hiyo ya kanisa lake wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa kukabidhi msaada huo.

Amesema walengwa ni watu wenye ulemavu na wasio na uwezo wa kununua viti hivyo ambavyo nchini hupatikana kwa gharama kubwa.

’’Walengwa wanatakiwa kuchukua fomu na kuzirudisha zikiwa zimegongwa mhuri wa kiongozi wa dini yoyote ile au wa kiongozi wa serikali ya mtaa.

’’Utaratibu huu utatumika ili kuzuia uwezekano wa mtu mmoja kuwa na baiskeli zaidi ya moja na hivyo kukosesha wengine,” amesema Askofu Kilimba.

Akasema walengwa 100 kati yao watatoka katika wilaya zote tatu za mkoa wa Dar es salaam.

Ameitaja mikoa mingine itakayofaidika na msaada huo kuwa ni Unguja, Pemba, Dodoma na Singida.

Kadhalika Askofu Kilimba ameongeza kuwa msaada huo pia utawanufaisha wasafiri na wagonjwa kwa kuwa baadhi ya viti hivyo hivyo vitatolewa kwenye viwanja vya ndege na hospitalini.

Pia kiongozi huyo ameitaka serikali iangalie uwezekano wa kupunguza kodi kwenye vifaa vya walemavu ili kuleta unafuu wa bei zake kwa walemavu.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.