20 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ofisa ’ala mkunjo’ baada ya kushtukia...
 
2006-10-20 14:36:43
Na Futuna Seleman, Temeke

Ofisa wa Vijana wa Manispaa ya Temeke, Bi. Alice Chale, alitoa kali na mpya baada ya ’kula mkunjo’ alipostukia ’zengwe’ lililoibuliwa dhidi yake katika kikao cha robo mwaka cha Halmashauri ya Baraza la madiwani wa Manispaa hiyo.

Bi Chale aliamua ’kula kona’ hiyo, mara baada ya kuingia katika kikao hicho akiwa amechelewa na kukuta ’zengwe’ la azimio la kumuondoa katika nafasi yake limeshapitishwa.

Sakata lenyewe lilikuwa hivi:Bi Alice akiwa hana hili wala lile aliingia katika kikao hicho akiwa amechelewa huku akiwa kabeba ’kithemometa’ chake kwapani na makabrasha yake mkononi.

Bi Alice wakati anaketi ndio azimio la kumuondoa madarakani lilikuwa limeshapitishwa na baraza hilo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya upotevu wa baiskeli zaidi ya 100 za vijana.

Lakini katika hali ya kushangaza Bi Alice aliketi kama dakika kumi hivi huku afisa mwenzake aliyekaa karibu naye akimpa ’akiba ya maneno’ ya maazimio ya kikao hicho dhidi ya ’zengwe’ lake lililokuwa ’likidiskasiwa’ muda mfupi baada ya kufika kwake.

Kuona hivyo, Bi Alice alichukua vifurushi vyake na kisha kutoka nje kama siyo yeye na kutokomea. Hadi kikao hicho kinamalizika hakurejea tena kikaoni.

Hata hiyo madiwani waliokuwa wakitoa hoja za kumlalamikia afisa huyo hawakumuona wakati anaingia hadi ’anakula mkunjo’.
Azimio la kumuondoa ofisa huyo wa ngazi nyeti ya juu kwa vijana lilichukuliwa na madiwani hao katika kikao chao kilichofanyika juzi.

Madiwani hao walitoa dukuduku lao wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo walimtuhumu bosi huyo wa vijana kufanya mambo kinyume na maadili ya kazi.

Baadhi ya tuhuma alizotupiwa ofisa huyo ni pamoja na ’kuyeyuka’ katika mazingira ya kutatanisha kwa baiskeli zaidi ya 100 za vijana wa Manispaa hiyo ambazo zilitolewa na wafadhili mbalimbali.

Diwani wa Kata ya Kurasini, Bw. Wilfred Kimatti, alisema uvumilivu waliokuwa nao kwa ofisa huyo, sasa umefikia kikomo kutokana na kile alichodai kuwa ni utendaji wake mbovu kiasi cha kusababisha vijana wengi sasa kukosa imani na Manispaa yao.

”Hii siyo mara ya kwanza kwa ofisa huyu kutaka kuondolewa, lakini tulimvumilia na kumuonea huruma, lakini sasa lazima ang’oke,” akasema.

Madiwani hao walitoa malalamiko hayo kwa nyakati tofauti kila mmoja.

Kwa upande wake akizungumza mara baada ya kikao hicho Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Jerome Bwanausi alisema kuwa hatua hiyo imetokana na ofisa huyo kuonekana kuwa hana uwezo wa kuongoza idara hiyo.

Akasema baraza lilimuomba Mkurugenzi kumteua ofisa mwingine kisha Bi Alice apewe kitengo kingine kwa vile amekuwa ni kikwazo cha maendeleo kwa vijana katika kata.

”Vijana wote wanamlalamikia, madiwani nao hivyo hivyo ni vema akambadilisha kitengo lakini si kwamba amefukuzwa kazi, akasema Meya Bwanaussi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.