20 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waziri wa JK aumbuka
 
2006-10-20 14:39:49
Na Mary Edward, PST- Kongwa

Naibu Waziri mmoja wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete amekumbwa na masahibu ya mwaka na ambayo pengine hatayasahau kirahisi katika historia ya kushika wadhifa wake huo wa juu.

Tukio hilo lililomfanya Mheshimiwa apigwe na bumbuwazi kwa mshangao wa dakika kadhaa ni lile la kujikuta akipokelewa na watu wawili pekee katika mojawapo ya ziara zake muhimu kikazi wilayani hapa.

Naibu Waziri huyo ni Bw. Charles Mlingwa wa Maendeleo ya Mifugo aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti wa Malisho ya Mifugo Kongwa.

Mbali na mambo mengine kadhaa yaliyomshangaza Bw. Mlingwa kituoni hapo, lile la kujikuta msafara wake ’mzito’ ukipokewa na watumishi wawili pekee wa kituo hicho ndilo lililozua mjadala wa aina yake na kumfanya hata yeye mwenyewe abaki akishangaa kwa muda, bila kuamini juu ya kile anachokishuhudia.

Kufuatia bumbuwazi hilo la Bw. Mlingwa juu ya kupokelewa na watumishi wawili pekee, wenyeji wake walilazimika kumueleza kile kilichosababisha hali hiyo isiyo ya kawaida.

Wakamfahamisha Bw. Mlingwa kuwa sababu ya kupokelewa na watumishi wawili na si wa idadi ambayo pengine aliifikiria inatokana na ukweli kuwa kituo hicho, licha ya ukubwa na umuhimu wake kwa maendeleo ya sekta ya mifugo nchini, bado kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi.

Akaelezwa Bw. Mlingwa kuwa upungufu wenyewe, umetokea kituoni hapo baada ya watumishi wengi ’kupigwa chini’ katika mpango maalum wa Serikali wa kupunguza idadi ya watafiti kituoni kwao hapo.

Akaelezwa Bw. Mlingwa na Ofisa Mfawidhi wa Kituo hicho Bw, Benard Jumbe kuwa pia, kituo chao hicho kimetelekezwa kwa muda mrefu ambapo mbali na kukabiliwa na upungufu wa watumishi, wanajikuta vilevile wakishindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yao kutokana na ukata uliokithiri na kuwa na vitendea kazi duni.

”Kwa zaidi ya miaka 10 kituo kina mtafiti mmoja tu ambaye pia ndiye mtawala wa kituo... Mhe. Naibu Waziri, upungufu huu unakwamisha shughuli nyingi za utafiti na ndio maana mwenyewe umeshuhudia leo hii ukipokelewa na watu wawili tu... hii ndiyo hali halisi iliyopo kituoni hapa,” akasema Bw. Jumbe ambaye pia alielezea hali mbaya ya uchakavu wa nyumba za kuishi vibarua wa kituo hicho.

Aidha alisema pia kituo hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikipata fedha kidogo kwa ajili ya kuendeshea kituo na kuongeza kuwa, hata pale ambapo pesa hizo zimepangwa kutolewa, imekuwa ni kawaida kucheleweshwa kufika kwao kwa wakati.

Kali zaidi, ikaelezwa kuwa licha ya kujihusisha na utafiti, kituo hicho ambacho kipo umbali wa kilomita 70 kutoka Dodoma Mjini, ni kwa muda mrefu sasa kimekuwa hakina mfumo wowote wa mawasiliano ya simu wala mtandao wa ’Internet’ kwa ajili ya kukiunganisha na makao makuu, hivyo kuwafanya wakose taarifa muhimu za kitafiti na zile zitokazo makao makuu.

Hata hivyo, akasema Bw. Jumbe kuwa pamoja na matatizo yote hayo, kituo chake kinaendelea na utafiti wa mimea ya malisho toka ndani na nje ya nchi.

Awali akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk. David Sendaro alikiri kuwepo uhaba wa wataalam katika kituo hicho na kusema kuwa suala hilo linashughulikiwa.

Naye Naibu Waziri, Bw. Mlingwa alionyesha wazi mshangao alioupata katika kituo hicho chenye jina kubwa pale linapozungumziwa suala la maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

”Hali ya hapa ni tofauti na jina kubwa la kituo,” akasema Bw. Mlingwa.

”Kituo gani hiki cha utafiti hakina hata mawasiliano ya simu au kompyuta tu? Haiwezekani, ni lazima mpatiwe angalau kompyuta,” akaongeza Bw. Mlingwa, hiyo ni baada ya kuelezwa kila kitu kuhusiana na matatizo mbalimbali yanayokikabili kituo hicho maarufu.

Pia alitoa changamoto kwa kuwataka watafiti wizarani kwake kuwa na mipango madhubuti ya kukiendeleza kituo hicho na pia kuwasaidia kwa karibu wafugaji wanaowazunguka.

”Tunahitaji ajenda ya kitaifa ya utafiti wa mifugo ili kupata sababu ya kuboresha vituo vyetu…haiwezekani tu ukasema unataka kufanya kitu fulani bila ya kuwa na ajenda.

Lazima tuwe na ajenda halafu ndiyo tuweze kutafuta fedha za kuitekeleza ajenda hiyo,” akasema Dk. Mlingwa.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.