|
Mameneja wa Airports wabadilike kulingana na teknolojia
2006-10-21 14:18:57
Na Aziz Issa
Naibu Waziri wa Miundombinu Dokta Maua Daftari amewataka mameneja wa viwanja vya ndege nchini kukidhi matakwa ya wateja na kubadilika kulingana na teknolojia.
Amesema mamlaka ya viwanja vya ndege nchini,TAA, inayo majukumu mengi katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amewaagiza kuongeza juhudi maradufu ili waweze kutoa huduma kwa kiwango kinachoridhisha na hivyo kukidhi ushindani wa kibiashara.
Amesema nafasi ya kufanya vizuri zaidi bado ipo hivyo waelekeze nguvu zao katika kuongeza ufanisi na mapato ili waweze kunufanikiwa zaidi kwa miaka ijayo.
Amesema wasafirishaji kwa njia ya anga wanahitaji huduma bora kwa usalama wa mali zao.
Hata hivyo, akasema hali ya miundombinu na vitendea kazi haviko katika hali nzuri na hata utoaji wa huduma hauridhishi.
Kwa upande wa mazingira, Dk. Maua amewataka kujiweka katika mazingira ya kuweza kushinda kibiashara kama yanavyofanya mataifa mengine duniani.
Pia amewataka kupanda miti katika bustani ili waweze kuwa na mahali pazuri pa kupumzikia abiria wakati wakisubiri usafiri.
|