|
Ponda, kunguruma Dar Baraza la Idd, JK kupasua anga Arusha
2006-10-21 14:21:02
Na Badru Kimwaga, Jijini
Wakati Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kunguruma mjini Arusha katika baraza la Idd lililoandaliwa na BAKWATA, masheikh maarufu nchini, Ponda Issa Ponda na Amiri wa Shura ya Maimamu, Sheikh Mussa Kundecha wao watanguruma katika baraza lao litakalofanyika Jijini Dar es Salaam.
Baraza la Idd la BAKWATA bado halijafahamika litafanyikia katika ukumbi gani, lakini lile la akina Sheikh Ponda, tayari limeshafahamika litafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Kwa mujibu wa vipeperushi na matangazo mbalimbali yaliyobandikwa misikitini na mitaani, baraza la Idd la akina Sheikh Ponda litafanyika kuanzia saa 10 jioni na litahudhuriwa na masheikh kadhaa wanaharakati.
Baraza hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Jumuiya ya Waislam Tanzania, litafanyika siku ya Idd, inayotarajiwa kuwa mapema wiki ijayo kulingana na mwandamo wa mwezi.
Vipeperushi na matangazo hayo ya baraza la Idd la wanaharakati hao limekuja siku chache baada ya BAKWATA kupitia mkurugenzi wake wa habari, Sheikh Selemani Gorogosi kutangaza kuwa swala ya Idd itaswaliwa mjini Arusha kati ya Okt 23 na 24.
Katika taarifa hiyo ya BAKWATA ni kwamba Rais Jakaya Kikwete ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika baraza la Idd litakalofanyika kwenye ukumbi utakaotangazwa baadaye.
|