21 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watanzania waliouawa Marekani
 
2006-10-21 14:22:34
Na Mwandishi Wetu, Jijini

Wakati misa ya kuwaombea Walter Mazula na mchumba wake Vonetha Nkya waliouawa huko Marekani mwezi uliopita inafanyika leo, vifo hivyo vimebaki kuwa fumbo miongoni mwa wengi huku ikiaminika kuwa muuaji angali akitesa kwenye mitaa ya miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Misa ya kuombea vijana hao waliouawa kikatili, imepangwa kufanyika leo saa 11:00 jioni kwenye kituo cha Vijana Don Bosco Upanga.

Ni kwa nini vijana hao wa Kitanzania wameuawa kule ugenini? Ni nani hasa kafanya ukatili wa kuwaua? Na kwa nini hadi leo hakuna taarifa zozote juu ya kutiwa mbaroni kwa mhalifu huyo?.

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo yamekuwa yakisumbua vichwa vya watu kwa siku ya 30 sasa tangu kuuawa kwa vijana hao Septemba 22 mwaka huu kule mjini Detroit na kisha kuzikwa pamoja katika makaburi ya Kinondoni Jijini Dar ya.

Hadi sasa hakuna taarifa rasmi za kukamatwa kwa mtekelezaji wa mauaji hayo ya kinyama, kitendo kinachowafanya watu waamini kuwa muuaji atakuwa akiendelea kula kuku kwa mrija.

Hali hiyo ya kutotolewa kwa taarifa za mwennendo wa suala hilo imezua wasiwasi kwa baadhi ya Wabongo walio na ndugu zao nje ya nchi, wakihofu kuwa huenda nao siku moja wakaletewa taarifa mbaya za kuuawa kwa ndugu zao na kisha mambo yakawa kimyakimya kama ilivyo kwa tukio hili la kusikitisha juu ya mauaji ya marehemu Mazula na mchumba wake Vonetha.

”Vifo vyao vinasikitisha... ni vyema Watanzania tukaondolewa hofu kwa kuelezwa kama muuaji ameshakamatwa ama la,” akasema Bi. Aisha Mohamed, mkazi wa Kijitonyama aliyedai kuwa mwanawe yuko nje ya nchi.

Lakini , wakati kukiwa hakuna taarifa rasmi zilizotolewa kwa umma juu ya sabahu za mauaji wala mwenendo wa sakata lenyewe, baadhi ya Wabongo wamekuwa wakizusha minong’ono tofauti kuhusiana na muuaji wa wachumba hao.

Mkazi mmoja wa Msasani ameiambia Alasiri kuwa ana ndugu yake amemtumia barua pepe inayoeleza kuwa eti, sababu ya mauaji ya vijana hao wachumba ni kisa cha mapenzi.

Anasema msimuliaji wa uvumi huo ambao pia Alasiri imebaini kuwa umesambaa kwa wengi kuwa baada ya marehemu Mazula na Vonetha kuwa wapenzi, kuna mwanaume mmoja asiyetajwa jina ambaye yeye hakufurahia mapenzi yao.

Zikasema taarifa hizo za uvumi kuwa kwa sababu hiyo, huyo mvamizi akatoa vitisho akitaka Vonetha amtose mchumba wake Mazula ili nafasi hiyo aitwaye yeye.

Hata hivyo, taarifa hizo zinasema kuwa Vonetha alikuwa makini na kuendelea kumpenda mchumba wake Mazula kwa moyo wake wote na kukataa kutetereka.

Kutokana na uamuzi huo wa mwanamke Vonetha, taarifa hizo za uvumi zinasema kuwa jamaa aliyelazimisha kupendwa yeye ndipo akatekeleza mpango wake wa mauaji kwa nia ya kuwakomoa wote wawili.

Hatahivyo, siku ya mazishi pale kwenye Viwanja vya Leaders Kinondoni, Baba Mzazi wa Walter, Kapteni Mazula, hakusema lolote kuhusu chanzo cha mauaji hayo.

Usiku wa siku hiyo ya Septemba 22, mwili wa Walter ukaokotwa ukiwa na majeraha ya risasi huku Vionetha akikutwa amefia kwenye gari iliyoungua huku mwili wake ukiwa umeharibika vibaya.

Ukweli wa kuuawa kwao ni upi? Bado ni fumbo ambalo bila shaka, upelelezi wa mamlaka husika za usalama nchini Marekani ukikamilika kila kitu kitakuwa bayana.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.