|
Nyumba hii balaa!
2006-10-21 14:23:08
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Ama kweli ukistaajabia ya Musa utaona ya filauni kama haya yaliyomkuta mpangaji wa nyumba moja hapa Jijini ambaye sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Nyumba hiyo iliyopo katika maeneo ya Jangwani Jijini Dar es Salaam masharti yake huwafanya wapangaji wajikute wakiwa kwenye wakati mgumu pale wanapokwenda kinyume na maelekezo ya baba mwenye nyumba wao.
Kijana Ahmed Maftah, 20, ni shahidi wa kile ambacho huweza kumtokea mpangaji anayeasi masharti ya kuishi katika nyumba hiyo.
Maftah amevunja kanuni mojawapo ya kumtaka mpangaji asiingize mwanamke ndani.
Baada ya kuasi masharti hayo na kuingiza demu ndani, amejikuta akiambulia kipigo kisicho cha kawaida kilichomfanya alazwe kama anavyoonekana pichani mbele.
Huku akiwa wodini na akiongea kwa shida, Maftah anasimulia sakata zima kama hivi: Siku ya tukio, kama walivyo vijana wengine wa hirimu yangu, alinitokea msichana wa wenyewe na baada ya kumsomesha vya kutosha, binti akanikubalia.
Baadaye, Maftah aliyekosa senti za kumpeleka mahala pazuri pa kujivinjari na mpenzi wake huyo, akaamua kwenda naye chumbani kwake.
Nikamuingiza chumbani kwa kuvizia. Baadaye tukaendelea na mambo yetu. Kumbe baba mwenye nyumba aliniona wakati nikiingia na mpenzi wangu huyo.
Ndipo bila kutarajia, akanivamia ghafla chumbani na kuanza kunipiga mfululizo kama mwizi.
Halafu ikawaje?
Yule mpenzi wangu hakuguswa, hivyo alipata mwanya akakimbia. Mie nilipigwa sana na damu zikaanza kunivuja.
Kwa bahati, nikachoropoka na kukimbilia Kituo cha Polisi Jangwani, kisha nikaletwa hospitali na hadi sasa hali yangu ndo kama unavyoiona, akasema kijana huyo aliyelazwa katika wodi namba 17, Jengo la Sewahaji pale Muhimbili.
|