|
Gogoro lingine la nyumba labisha hodi kwa Magufuli
2006-10-21 14:24:08
Na Usu-Emma Sindila, Mikocheni.
Wakati akiwa katikati ya kimbembe kizito cha migogoro ya nyumba na ardhi, gogoro lingine zito limebisha hodi mlangoni mwa Waziri John Pombe Magufuli.
Gogoro hilo linahusu nyumba namba 435 iliyoko Block 43 Part 1 pale Kijitonyama, Jijini.
Katikati ya sakata hilo, yumo Bi. Asia Hassan Ramadhani anayedai kudhulumiwa nyumba ya urithi ya marehemu baba yake.
Akiongea na gazeti hili, mwanamama huyo amesema ameamua kumlilia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Magufuli akiamini kuwa ndiye mtu pekee mwenye uwezo wa kuingilia kati na sakata hilo na kumwezesha kupata haki yake.
Amedai kuwa mgogoro huo ulianza tangu mwaka 1989 wakati baba yake alipofariki dunia hadi hivi sasa na hakuna haki yoyote iliyopatikana licha ya kuzunguka katika vyombo kadhaa vya sheria kutafuta usuluhishi.
Amesema chanzo cha mgogoro huo ni mtu mmoja ayedaiwa kughushi sahihi za marehemu na kudai kuwa aliuziwa nyumba hiyo na marehemu baba yake Mzee Hassani Ramadhani Seif wakati akijua kuwa si kweli.
Bi Asia amesema amefikia uamuzi wa kuomba msaada wa Bw. Magufuli baada ya kuona jitihada zake za kutafuta haki kwa njia nyingine kushindikana kabisa na hivyo kushindwa kupata haki yake.
Amesema amewahi kupeleka malalamiko yake hayo kwa viongozi kadhaa pamoja na mahakama lakini bado hakupata msaada wowote kwa kile alichodai kuwa mtu anayemtuhumu aliongea na wasimamizi wa kesi hiyo.
Amedai kiwanja hicho kiliachwa na marehemu baba yake Mzee Hassan Ramadhani Seif na baadaye familia kumkabidhi yeye awe msimamizi wa mali hiyo.
Enzi za uhai baba alikinunua kiwanja hicho toka Serikalini mwaka 1977 na baada ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa alikabidhiwa kiwanja hicho pamoja na hati zake zote na kisha kuanza ujenzi ambao alifanikiwa kuumaliza kabla hajaaga dunia mwaka 1989, akasema Bi. Asia.
Anasema kuwa baada ya kumzika baba yake kijijini kwao Kondoa walirejea jijini na kujitayarisha kwa ajili ya kuhamia katika nyumba yao hiyo lakini walipofika hapo walikuta nyumba hiyo tayari ikiwa na wakazi ndani yake.
Tulishangaa sana kukuta kuna watu wapo katika nyumba yetu, hivyo tukaamua kwenda kwa mjumbe na kumueleza kinachoendelea ambapo hata yeye alishangaa sana na kutushauri kupeleka suala hili CCM, akasema Bi. Asia.
Bi. Asia akaongeza kuwa, baada ya kulifikisha suala hilo huko, viongozi wa CCM walituambia tupeleke hati halisi za mali hiyo na kisha wakatuambia kurudi baada ya siku mbili, lakini cha ajabu ikawa ndio tumechochea moto zaidi, kwani hakuna chochote kilichofanyika zaidi ya kuzungushwa tangu mwaka 1989 hadi 1991, akaongeza.
Amedai baada ya kuona wanazidi kuzungushwa waliamua kutafuta msaada mahali pengine ambapo safari hii waliangukia Ikulu hata hivyo pamoja na kupata msaada mkubwa lakini bado haikusaidia kwani tatizo hilo lilirudishwa polisi na hadi sasa hakuna haki iliyopatikana.
|