|
Idd hiyoo! Viwalo navyo vyapanda bei maradufu
2006-10-23 17:23:20
Na Futuna Seleman,Kariakoo
Bei ya viwalo vya watoto katika maduka ya nguo Kariakoo jijini Dar es Salaam imepanda kufuatia sikukuu ya Id Elfitri inayotarajiwa kufanyika kesho kutegemea kuandama kwa mwezi.
Alasiri iliwashuhudia akinamama wengi wakiwa madukani kusaka nguo za watoto huku wakilalama kutokana na kupanda kwa bei ya nguo hizo.
Mama Ashura wa Temeke anasema amenunua nguo za binti yake kwa shilingi 18,000 kila moja wakati nguo hizo zamani ungeweza kuzipata kwa shilingi 8,000 hadi 9,000.
Naye Mama Rashid Mkilalu wa Vingunguti anasema nguo za watoto wa kike zina bei ile mbaya tofuuti na siku za kawaida wanapokwenda kununua nguo hizo.
Kwa vile ni sikukuu nimewanunulia wanangu hebu fikiria nguo moja shilingi 20,000 sisi wengine ni walalahoi inatubidi tununue hivyo hivyo kuwafurahisha watoto siku za kawaida tunauziwa nguo hizi hizi kwa shilingi 10,000,akasema Mama Rashid.
Naye Mama Ahmed Saleh wa Tabata Liwiti amesema nguo za watoto wa kiume ni adimu sana tofauti na za watoto wa kike na bei yake nayo kwa sasa imepanda.
Pensi jinsi na tisheti yake inauzwa hadi elfu 15 kwa zile za kawaida lakini ukizikuta zile kali kabisa hiyo bei ni hatari akasema Mama Medi.
Hata hivyo baadhi ya akinamama wamesema kuwa wanaona ni kawaida kwa vile kila mwaka hali kama hiyo hutokea na wenye maduka kwa upande wao huwa mwaka wa mavuno kwao.
Wakati huohuo, bei ya futari katika soko Temeke Stereo imeshuka tofauti na ilivyoanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Magimbi yaliyokuwa yakiuzwa kwa bei ya shilingi 500 hadi Sh.1,000 sasa yanauzwa fungu shilingi 100, 200 hadi Sh.300 ambapo viazi vitamu vilivyokuwa vikiuzwa kwa fungu 500 hadi 1,000 sasa vimeshuka hadi kufikia Sh.100, 200 hadi 300.
Tambi ambazo zilikuwa zikiuzwa kilo Sh.1,000 nazo zimeshuka hadi kufikia Sh.600 huku maboga nayo yameshuka hadi kufikia Sh.300 badala ya 700.
|