23 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Adakwa laivu Jangwani akipora kwa pisto
 
2006-10-23 17:28:40
Na Emmanuel Lengwa na Magreth Simba, Jijini

Mtu mmoja anayesadikiwa kuwa ni mnyang’anyi anashikiliwa na Polisi kwa kukutwa na bastola. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Bw. Masindoki Masindoki amesema mtu huyo ambaye jina lake halikufahamika, amekamatwa baada ya ushirikiano wa wananchi na polisi wa Kituo cha Jangwani majira ya saa 11:15 alfajiri leo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Masindoki amesema alfajiri hiyo, Bw. Abdallah Awadh ambaye anafanya kazi katika Kampuni ya Scandnavia, alidamka kuwahi lakini akiwa njiani maeneo ya Jangwani, alivamiwa na kundi la vibaka watano na kuporwa simu na fedha kiasi cha sh.90,000.

Akasema Bw. Masindoki kuwa baada ya kuporwa, Awadh akapiga kelele na ndipo wananchi waliokuwa karibu na askari wa kituo cha Jangwani walipojitokeza kuwafukuza waporaji hao na kumnasa mmoja wao.

Kamanda Msindoki akasema kuwa baada ya kupekuliwa, mporaji huyo akakutwa na bastola moja aina ya Baretta na risasi sita.

Amesema uchunguzi wa awali ambao bado haujathibitika unaonyesha kuwa silaha hiyo ni mali ya Shaban Said ambaye aliibiwa siku za nyuma.

Katika tukio jingine, moto mkubwa umezuka na kuteketeza banda la kuhifadhia chupa tupu za plastiki zilizotumika katika kiwanda cha Unido, Msasani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni Bw. Jamal Rwambow amesema tukio hilo lilitokea jana mchana kiwandani hapo.

Akasema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.
Pia Kamanda Rwambow amesema mtu mmoja amekufa baada ya kugongwa na gari katika maeneo ya Mkwajuni barabara ya Kawawa jijini.

Amesema gari lililomgonga mtu huyo halijafahamika kwa vile dereva alikimbia baada ya ajali hiyo.

Mwili wa mtu huyo ambaye pia hajafahamika umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Wakati huo huo wakazi wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuwa watulivu na kusherehekea kwa amani sikuu ya Idd-El Fitr.

Kamanda Rwambow amesema vijana wake tayari wamejipanga vema kuhakikisha sikukuu hiyo inasherehekewa kwa amani katika Mkoa wake.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke Emmanuel Kandihabi amewataka wakazi wa wilaya ya Temeke kutowaacha watoto wadogo wazurure peke yao wakati wa kusherehekea sikukuu hiyo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.