|
Majambazi yafanya kufuru
2006-10-23 17:29:22
Na Peter Cassonga, PST-Kigoma
Majambazi mkoani hapa yanaendelea kufanya kufuru kila kukicha ndani ya Ziwa Tanganyika mkoani hapa na tayari yameshasababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Kama hiyo haitoshi, majambazi hayo yamekuwa yakiwafanya watumiaji wa ziwa hilo la bonde la ufa kukosa amani huku biashara zikitatizwa, uvuvi ukifanyika kwa hofu na pia kuhatarisha shughuli nyingine kadhaa za kiuchumi ndani ya ziwa hilo.
Taarifa inayozungumzia hali hiyo mbaya imetolewa na Mkuu wa Mkoa huu Bw. Joseph Simbakalia.
Amesema mkuu huyo kuwa kutokana na hali tete inayosababishwa na uporahi wa kila mara unaofanywa na majambazi, tayari zana za uvuvi zenye thamani ya shilingi milioni 21.4 zimeshapotea baada ya kukwapuliwa na watu hao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Bw. Simbakalia amezitaja zana hizo ambao zimekuwa zikiporwa sana na majambazi wanaodhaniwa kuwa ni waasi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Kongo (DRC) kuwa ni pamoja na boti (vipe), mashine za boti, nyavu za kuvulia, karabai, kamba za kufungia, mafuta ya kuendeshea mashine na madumu ya kuhifadhia mashine hizo.
Akasema Bw. Simbakalia kuwa kuporwa kwa zana hizo kumewafanya wavuvi wengi kutokuwa na moyo wa kuwekeza katika kutumia zana bora na hivyo kufanya kazi ya uvuvi isiwe na tija ya kutosha.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa mkoa ameiomba serikali kuu kupitia wizara zake husika iimarishe ulinzi katika ziwa hilo kwa kuweka boti ziendazo kasi kuimarisha doria ili kuweka mazingira mazuri kwa wavuvi kufanya shughuli zao.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa kuporwa kwa zana hizo za uvuvi na hali ya usalama usioridhisha katika nchi za maziwa makuu ni miongoni mwa changamoto zinazodumaza mkoa wa Kigoma kiuchumi na kwamba kuimarika kwa hali ya usalama katika nchi hizo, kutaleta nafuu ya kiuchumi mkoani humo.
|