23 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

DC amuoza mwanafunzi kwa Mdosi
 
2006-10-23 17:30:10
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Wakati Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali yakipinga watoto wa kike kuozeshwa wakiwa na umri mdogo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam imefungisha ndoa mtoto mwenye umri wa miaka 13.

Ndoa hiyo ni kati ya mtoto Khudeija Mkanji, 13, na mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Kiasia aitwaye Shafic Dhala.

Ndoa hiyo ilifungwa Agosti 3 mwaka jana na kupewa cheti cha ndoa chenye namba B No.0385853, Alasiri imebaini.

Akithibitisha taarifa hiyo, baba mkubwa wa binti huyo, Bw. Amirali Khanji amesema chanzo cha binti wao kuozeshwa akiwa na umri mdogo ni kutengana kwa wazazi wa binti huyo.

Amedai kuwa baada ya wazazi wake kutengana, mama yake aliamua kumuozesha kwa siri ili kumkomoa baba yake.

”Mtoto huyo ameozeshwa na mama yake bila ridhaa ya baba baada ya kutoelewana kati yao na kutengana, lengo la mama yake ni kumkomoa baba wa mtoto asiambulie chochote,” akadai Bw. Khanji.

Amedai kuwa mama mzazi wa binti huyo alimdanganya Mkuu wa Wilaya juu ya umri wa binti wao na kusema kuwa ana miaka 19 badala ya 13.

Kwa mujibu wa baba mkubwa wa binti huyo, kutokana na sababu ambazo hazijahamika hadi leo, ndoa hiyo haikufuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutangazwa kwa siku 21 kama inavyoelekezwa na sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Bw. Khanji amesema kuwa baada ya kubaini hujuma hiyo alibisha hodi katika ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya kulalamika na kuwasilisha vielelezo vyote vinavyoonyesha kuwa binti wao bado ana umri mdogo usioruhusiwa kisheria kuolewa.

”Nilimpelekea Mkuu wa Wilaya vielelezo vyote ikiwa ni pamoja na cheti cha kuzaliwa cha mwanangu na barua ya mwalimu wake mkuu maana alikuwa bado ni mwanafunzi,” akasema.

Cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo ambacho Alasiri ina nakala yake kinaonyesha alizaliwa Juni 7, 1992.
Amedai kuwa baada ya Mkuu wa Wilaya kupitia vielelezo vyote na kufanya uchunguzi wa kina alikiri kuwa Msajili wa Wilaya hiyo alipotoshwa na taarifa ya uongo aliyopewa na hivyo kufungisha ndoa kinyume cha matakwa ya sheria ya ndoa.

Kufuatia kubainika kwa hali hiyo, Ofisi ya Katibu Tawala ya Manispaa ya Ilala ilimwandikia barua Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Ilala ili aivunje ndoa hiyo haraka iwezekanavyo.

Sehemu ya barua hiyo ambayo Alasiri inayo nakala yake inasema hivi:

Ndoa hiyo ilistahili kufungwa kwa kibali maalumu cha Msajili wa Ndoa, kwa kuwa haikutangazwa kwa muda wa siku 21. Hivyo, ndoa hiyo haikuwa na kibali.

Wahusika walidanganya umri wa bibi harusi (Khudeija Mohamed Taki) kuwa ana miaka 19. Aidha, baadaye imebainika kuwa binti huyo ana umri wa miaka 13 kufuatia baba yake mzazi kuwasilisha cheti cha kuzaliwa cha binti yake.

Kwa Mujibu wa kifungu Na. 24 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, msichana mwenye umri wa chini ya miaka 18 endapo atatakiwa kuolewa atatakiwa kupata ridhaa ya wazazi wake wote wawili. Ridhaa hiyo haikupatikana.

Msajili /Khadhi wa Wilaya alipotoshwa na taarifa ya karani wake na hivyo kufungisha ndoa hiyo kinyume cha matakwa ya ndoa.

Aidha kutokana na Ofisi hii kupokea malalamiko toka kwa mzazi na baadaye kufanyika uchambuzi juu ya ndoa hiyo, imebainika wazi kuwa ndoa hiyo imefungwa kinyume cha sheria ya ndoa (1971) na hivyo tunawasilisha walaka huu wenye azma ya kufuta ndoa hiyo iliyofungwa tarehe 3 Agosti 2005.

Kwa mujibu wa baba huyo, binti huyo ambaye alitakiwa mwaka huu awe kidato cha pili katika shule moja hapa Jijini tayari amebeba mimba na kujifungua mtoto.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.