|
Magufuli awakabidhi rungu wananchi wasiojua sheria
2006-10-26 15:18:30
Na USU-EMMA SINDILA, BAGAMOYO
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bwana John Magufuli amewapa rungu wananchi la kuwapiga nalo watu watakaobainika kutaka kuwadhulumu ardhi yao bila kuwapa fidia.
Waziri Magufuli amewakabidhi rungu hilo wananchi wa kijiji cha Zinga, Bagamoyo.
Rungu lenyewe ni sheria ya ardhi namba nne na tano ya mwaka 1999 inayosema ni lazima kila mwananchi atakayetoa ardhi kwa ajili ya kupimwa au kuendelezwa kulipwa fidia kwa wananchi.
Ishikeni kwa umakini mkubwa sheria hii ya ardhi namba nne kipengele cha tatu kifungu g pamoja na ile ya namba tano kipengele cha tatu kifungu cha g ili atakapokuja mtu na kupima ardhi yako kwa ajili ya maendeleo bila kukupa fidia uidai, akasema Bw. Magufuli.
Tena unamweleza kuwa huondoki mpaka umepewa fidia yako kwa kumweleza sheria hiyo, tena unamweleza na shingo unaipindisha kulee huku ukipiga mluzi, akasisitiza.
Nasema wanaochukuliwa mashamba na viwanja vyao ni lazima walipwe fidia, na wale wanaotaka viwanja ni lazima watoe fedha ili kuvipata…hapa ni fedha kwa fedha, akasema.
Katika kudhihirisha kuwa Bw. Magufuli hana utani na kazi yake aliwanyanyua Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo pamoja na Mkuu wa Idara ya Upimaji Ardhi wa UCLASS, ambaye ni mkandarasi katika kupima mradi wa viwanja 3000 wa mwaka 2003 ambao bado haujakamilika, kujibu malalamiko ya wananchi juu ya ucheleweshaji wa kukabidhiwa viwanja vyao.
Akijibu swali hilo Afisa Ardhi wa wilaya ya Bagamoyo, Bw. Michael Mlyambongo alisema zoezi hili limeshindwa kukamilika kutokana na mkandarasi kushindwa kufanya kazi katika mazingira ya mvua kwa muda mrefu.
Hata hivyo ameahidi kuwa watu hao watakabidhiwa viwanja hivyo baada ya wiki mbili.
Naye Mkuu wa Idara ya Upimaji ya UCLASS Bw. Kagai Martin alisema mradi huo ulichelewa kutokana na wanachi kutokukubali kutoa ardhi pamoja na kungoa vigingi vya mawe walivyokuwa wameweka kwa ajili ya ramani.
Aidha alisema mabadiliko katika sheria ya ardhi nayo yameathiri kwa kiasi na kusema kuwa pindi upimaji utakapokamilika utapelekwa wizarani kwa ajili ya uhakiki kisha kugawiwa kwa wananchi ndani ya wiki mbili.
|