|
Mtemvu ataka matumizi bora ya kisima alichozindua Tandika
2006-10-26 15:19:16
Na Haji Mbaruku, Jijini
Mbunge wa jimbo la Temeke, Bw.Abbas Mtemvu amezindua kisima cha maji kinachotarajiwa kupunguza tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wa Kata ya Azimio kule Tandika na maeneo ya jirani na eneo hilo Jijini Dar.
Wakazi wa kata hiyo waliwahi kumlalamikia mbunge huyo kuwa maji ni tatizo kubwa katika kata yao.
Bw.Mtemvu hata hivyo aliwaambia wakazi hao kuwa wawe walinzi wazuri wa kisima hicho ili kisije kikaharibika kwa muda mfupi.
Nitashangaa sana kuona watu wamengoa mabati na kuharibu kisima hiki, amesema mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Kisima hiki ni mali yenu, mlikuwa mnasumbuka na sasa nawaombeni mkitumie vizuri ili kiweze kudumu, amesema mbunge huyo kuwaambia wakazi wa eneo hilo wakati wa sherehe za uzinduzi.
Katika sherehe hiyo, pia Bw.Mtemvu aliwaonya baadhi ya watu wenye tabia ya kuchafua vyanzo vya maji na kusema kuwa wanastahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
|