|
Ajali yaua watatu, kujeruhi watano
2006-10-26 15:20:07
Na Sabina Mgela, Temeke
Watu watatu wamefariki dunia papo hapo na wengine watano kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka.
Licha ya kuua na kujeruhi abiria wake, gari hilo aina ya Mitsubish lenye nambari za usajili T676 ATL limeparamia kibanda cha chips na kukizoa na kisha kugonga masanduku matano ya soda.
Kaimu Kamanda wa Polisi wilaya ya Temeke, Emmanuel Kandihabi amesema ajali hiyo ilitokea jana saa 5:30 asubuhi huko Kongowe .
Akielezea ajali hiyo, Kamanda Kandihabi amesema dereva wa gari hilo ambaye hajajulikana, alikosa mwelekeo na kutoka nje ya barabara baada ya gari kumshinda wakati anajaribu kuovertake gari lingine.
Akasema kutokana na kuyumba yumba kwa gari hilo, dereva alijikuta akitoka nje ya barabara ambako aliparamia kibanda hicho cha chips mali ya mtu aliyetajwa kwa jina moja la Thabit.
Kwa mujibu wa Kamanda Kandihabi, dereva katika harakati za kujiokoa, alijaribu kulirudisha gari barabarani lakini akajikuta akigonga gari lingine aina ya Nissan Civilian lenye nambari za usajili T560 APD.
Kamanda amesema Nissan hiyo iliyokuwa ikitokea Kongowe kwenda Kigamboni ilikuwa ikiendeshwa na dereva Juma Shaha.
Baada ya kugonga Nissan, gari hilo lilipinduka na kuua abiria wake watatu papo hapo na wengine watano wameumia vibaya, akasema Kamanda Kandihabi.
Amesema dereva aliyesababisha ajali, aliingia mitini baada ya kuona mambo yameharibika na hadi sasa hajulikani aliko.
Kamanda amesema majeruhi wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako wamelazwa wakiwa wameumia vibaya.
Amewataka waliojeruhiwa kuwa ni Mohamed Kondo, 30, Juma Ali, 22, Salum Mohamed, 26, Suleiman Said, 25 na Ali Said, 20 wote wakazi wa Mongola Ndege.
Amesema watu waliopoteza maisha yao bado hawajatambuliwa.
|