|
Waliokwenda kujichana Idd Kigamboni...
2006-10-26 15:20:55
Na Waandishi Wetu, Jijini
Waswahili husema hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro.
Na ndivyo ilivyokuwa wakati wa kuadhimisha sherehe za Sikukuu ya Idd iliyofikia tamati jana ambapo licha ya raha zake, kumekuwa na matukio kadhaa yasiyokuwa ya kufurahisha huku vilio na simanzi vikitawala katika baadhi ya maeneo.
Katika moja ya matukio yaliyotokea wakati wa sherehe hizo ni kitimtimu cha aina yake kilichozuka jana jioni kwenye kivuko cha Kigamboni wakati watu waliokwenda kujirusha fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Kigamboni walipojikuta wakiwa roho mkononi.
Kitimtim hicho kilishababisha baadhi ya abiria waliokuwa wakigombania kupanda vivuko vya Mv. Kigamboni na Alina kupata michubuko kadhaa mwilini, akiwemo mama na mtoto mdogo waliokuwa wakigaagaa chini hadi walipookolewa na watu wa huduma ya kwanza.
Mpambano huo ulitokana na wingi wa abiria katika eneo hilo la kivuko upande wa Kigamboni.
Idadi hiyo ya abiria ilisababisha kusukumizana mlangoni huku watu wakikanyagana na kuumizana ambapo inasemekana watoto watatu walipoteza fahamu baada ya kukanyagwa au kubanwa katika vurugu hizo.
Hata hivyo baadaye boti ndogo iliyoandikwa Rescue SAR 1 ilifika katika eneo hilo la upande wa Kigamboni na wahudumu wawili wa kiume wakashuka na kuwachukua majeruhi hao.
|