|
Teksi bubu wasanii! Si mchezo
2006-10-27 19:20:59
Na Jacqueline Mosha, Jijini
Baadhi ya madereva wa teksi bubu zilizopo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamebuni njia ya kujipatia pesa za chapchap kwa kugeuza magari yao kuwa kama daladala hivyo kuepuka mtindo wa kusubiri abiria kwa foleni vituoni ambao unapoteza muda mwingi.
Wakiongea na Alasiri kwa nyakati tofauti, madereva teksi hao wamedai kuwa hivi sasa wamebuni njia hiyo ya kuchukua abiria vituoni hasa nyakati za asubuhi na jioni ambapo vituoni kunakuwa na msongamano wa abiria wengi na usafiri wa daladala huwa mgumu pia.
Sio siri siku hizi badala ya kukosa kabisa pesa za matumizi na ya kumpelekea tajiri jioni, tumeamua ni vyema tutumie njia hiyo ya kubeba abiria tofauti tofauti kwenye gari kama wafanyavyo watu wa daladala ili kukidhi mahitaji yetu, akasema Bw. Shomary Amri dereva wa teksi bubu inayoegeshwa eneo la Kariakoo.
Bw. Shomary amesema kuwa mtindo huo waliuanza kama mzaha lakini umeonyesha mafanikio na kuwapatia kipato cha kutosha hasa baada ya kulegeza nauli kwa kila kichwa kuanzia Sh. 500 au 1,000 ambapo nauli huongezeka kulingana na umbali anaokwenda mteja.
Anasema kuwa abiria wengi wanapokuwa vituoni asubuhi au jioni hupata shida ya usafiri kwavile daladala nyingi huishia njiani hivyo kusababisha watu kurundikana vituoni wakisubiri daladala na pindi linapotokea daladala moja hugombaniwa na kujaza abiria kupita kiasi.
Mbinu hii imesaidia wale wasioweza kugombea daladala wakati wa asubuhi na jioni vituoni, ndio maana tumeamua kuwapunguzia nauli ya teksi na huwa tunabeba watu wanaokwenda njia moja ingawaje huwa wanatoka sehemu tofauti, akasema Bw. Joachim John, anayeegesha teksi kituo cha Magomeni.
Bw. Joachim akasema ingawaje mbinu hiyo si rasmi lakini kutokana na ubunifu huo wa kusaka pesa za haraka, tayari baadhi ya maderava wa teksi bubu hizo wamejiwekea mkakati wa usalama wao na abiria wanaowabeba ili kuwaepusha na tatizo la kutekwa au kuvamiwa wawapo njiani hasa nyakati za jioni wanaporudisha wateja.
Huwa tunawashusha vituoni kwao kutegemea na njia tunayopitia, lakini tumeshajihami kwa kuwa makini na abiria wetu hasa tunapowabeba nyakati za jioni ili tusipatwe na matatizo ya kuvamiwa au kusumbuliwa, huwa tunakuwa makini kwa hilo, akasema Bw. Joachim.
|