|
Wanawake wa CCM Ilala wafundishwa ujasiriamali
2006-11-01 16:30:39
Na Sharon Sauwa, Posta
Wanawake katika Chama Cha Mapinduzi kutoka kata 22 za wilaya ya Ilala Jijini Dar wamenufaika na mafunzo ya ujasiriamali ambayo yatawawezesha kutopoteza mali zao kutokana na kushindwa kulipa mikopo.
Akizungumza na Alasiri Jijini, Diwani wa Viti maalum Bi. Ritta Kabati, amesema: Ukosefu wa elimu ya ujasiriamali imeonekana kuwa ni kikwazo kikubwa katika mafanikio ya akina mama na vikundi vyao... mafunzo haya yatakuwa na msaada mkubwa sana.
Akasema Bi. Ritta kuwa miongoni mwa vikwazo ni upande wa mikopo iliyoshindikana kulipika na sababu kubwa imedhihirika kuwa ni kutokana na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali.
Akasema hali hiyo imesababisha wanawake wengi kupoteza mali zao na kuwafanya wengine kuingiwa hofu katika kukopa na hivyo kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Bi. Kabati ameandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na madiwani wengine wa viti maalum katika manispaa hiyo ambao ni Bi. Eva Nyamoyo na Bi. Aisha Sururu.
|