|
Visa vya nyumba za Dar! Wapangaji watatu wapigwa notisi ya siku nne
2006-11-01 16:33:19
Na Valery Kiyungu, Jijini
Chama cha wenye nyumba nchini (CHAWENYUTA), kimepinga uamuzi wa mwenye nyumba, Bwana Mohammed Salehe wa Manzese Uzuri Jijini wa kuwapiga notisi ya siku nne wapangaji wake watatu.
Badala yake chama hicho kimemtaka mwenye nyumba huyo kuwapa wapangaji wake taarifa (notisi) ya miezi mitatu , kama sheria ya Chawenyuta ya mwaka 1984 inayoelekeza.
Chama hicho kimepinga maamuzi hayo kupitia baraza lake la usuluhishi ambalo liliketi chini ya Katibu wake wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Shaaban Mgana na mjumbe.
Baraza langu linapinga vikali hatua yako kuwapa wapangaji notisi ya siku nne, badala yake unatakiwa kuwapa miezi mitatu, ili nao waweze kujiandaa kwa zoezi la kuhama, Bw. Mgana akamwambia mwenye nyumba huyo.
Aidha Bw. Mgana amesema licha ya ukweli kwamba nyumba ni mali ya mlalamikiwa lakini ni vyema taratibu za sheria zitumike pale mwenye nyumba anapohitaji chumba ama nyumba yake kutoka kwa mpangaji.
Amesema utaratibu wa chama chake kumpa mpangaji notisi ya miezi mitatu unalenga katika kumwezesha mlengwa kutafuta chumba mbadala.
Baraza hilo liliketi kusikiliza shauri ambalo lilifunguliwa na wapangaji watatu dhidi ya mwenye nyumba wao Bw. Salehe, wakimlalamikia kuwapa notisi ya siku nne.
Wapangaji hao ni mabibi Mkiwa Rajabu, Hadija Omari na Bw. Saidi Omari ambapo kila mmoja anamiliki chumba kimoja kwa kodi ya Sh. 5,000.
Katika malalamiko yao wapangaji hao wamedai kuwa mwenye nyumba wao amewapa siku nne ili wahame kwenye nyumba, baada ya mwenye nyumba wao huyo kuuza nyumba yake.
Ametuambia tuhame kwenye nyumba yake ndani ya siku nne, kwani nyumba yake ameuza, akasema Bi. Mkiwa.
Amesema kibaya zaidi ni pale alipouza nyumba yake pasipo kuwapa taarifa, kwa maelezo kuwa waligundua hilo baada ya kuona mwenye nyumba mpya anahamia, huku yeye Bw. Salehe akiowatangazia kwamba baada ya siku nne wawe wamehama kwenye nyumba yake.
Katika utetezi wake mwenye nyumba huyo, Bw. Salehe amesema amekubali agizo la chama kuwapa wapangaji miezi mitatu, kuanzia Oktoba 23, hadi Januari 23, mwaka 2007.
Aidha amesema kuwa hakuelewa kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuwapa taarifa mapema wapangaji wakati alipokuwa na nia ya kuuza nyumba yake kwa maelezo kuwa nyumba ni mali yake.
|