|
Uporaji mpya wa viselula watua Dar
2006-11-01 16:36:27
Na Maabad Msuya, Jijini
Wajazi Jijini Dar es Salaam wametakiwa kuwa makini na aina mpya ya uporaji ambapo mwanaume humvizia mwanamke akiongea na simu na kisha humtokea na kujifanya mumewe na kumnyanganya kwa kisingizio kuwa anaongea na mabwana wengine.
Kama vile haitoshi, baada ya jamaa kunyanganya bibie simu ghafla hutokea mijamaa mingine ambapo nayo hujaribu kusawazisha mambo kwa kudai kuwa bibie huyo ni shemeji yao na walishamkanya kuhusu suala la kuongea na simu za mabwana zake.
Waliokumbwa na sakata hilo wanasema dili hiyo huweza kuwazuga watu ili wasiingilie.
Akiongea na Alasiri, bibie mmoja aliyekumbwa na mkasa huo amesema siku ya tukio akiwa katika kituo cha daladala pale Tazara mara alisikia kiselula chake kikiita katika mkoba na alipokichomoa akaanza kuongea na ndugu yake aliyempigia.
Akasema, wakati akiendelea kuongea na simu mara walitokea vijana kadhaa na mmoja kati yao akamnyanganya simu yake huku akijifanya ni mumewe ambapo alianza kumfokea akimtuhumu kuongea na mabwana wa nje.
Akiendelea kusimulia mkasa huo mwanadada huyo ambaye amesema nia yake ni kuwatahadharisha watu wengine akasema, kabla yule jamaa hajampora simu yake kwanza alianza kuzuga watu kwa kumshushia bibie huyo kipigo kitakatifu huku akimshutumu kuwa siku hizi amekuwa si muaminifu katika ndoa yao.
Kwa kweli kipigo alichonipiga yule kibaka nilishindwa kujizuia kulia na ndipo walipotokea watu wengine na kujifanya kuwa wao ni mashemeji zangu na wakaanza kusema, shemeji unaona sasa yaliyokupata sisi tulikukataza kuongea na simu za namna hiyo hukutusikia, akasimulia dada huyo.
Akasema, wale jamaa baada ya kutimiza azma yao walitokomea huku yeye akibaki akiangua kilio bila msaada wowote kutoka kwa watu waliohofika kuingilia wakidhani ni ugomvi wa wanandoa.
Mwanadada huyo amewatahadharisha wakazi wa Jijini hapa hasa wanawake kuwa makini na mbinu hiyo mpya ya vibaka ambapo humuibia mtu kiulaini.
|