|
Kaburu Orijino afariki Dunia
2006-11-01 16:38:19
Na Maabad Msuya, Jijini
Pieter Willem Botha, alikuwa ndiye sura ya Afrika Kusini ya weupe alipokuwa Rais wakati wa hatua za mwisho za mapambano dhidi ya ubaguzi.
Alikuwa akijulikana sana kama P.W.
Alichaguliwa kuingia Bungeni mwaka 1948, akateuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi mwaka 1966 na akatumikia kama Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1978 hadi 1984.
Akiwa katika wadhifa huo, Afrika Kusini iliendeleza kwa siri programu ya nyuklia kwa kushirikiana na Israel.
- Mwaka 1984, kufuatia mabadiliko ya kikatiba aliyoyapendekeza, Botha alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa taifa hilo.
Staili ya utawala wake iliwekwa bayana kwenye hotuba yake ya mwaka 1986 iliyojulikana kama Crossing the Rubicon Speech ambapo alipuuzia miito ya kimataifa kama ile ya kumuachia huru Nelson Mandela.
- Botha alitolewa kwenye nafasi yake hiyo na uasi uliofanywa na baraza la mawaziri mwaka 1989 na baadaye nafasi yake kuchukuliwa na F.W. de Klerk, ambaye alibadili mambo mengi yaliyokuwa yakipendelewa na wale wenye msimamo mkali, ikiwa ni pamoja na sheria ambazo zilikuwa ndizo msingi wa ubaguzi.
-Japokuwa majeshi ya usalama ya Botha yaliua zaidi ya watu 2,000 na inakisiwa watu wengine 25,000 waliwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka na mara nyingi wakiwa wameteswa, alikataa kuomba radhi kwa ubaguzi na alikanusha akidai alikuwa hajui chochote kuhusiana na utesaji na mauaji yaliyofanywa.
-Alikataa kutokea wakati alipoitwa na Tume ya Ukweli na Usuluhishi iliyosimamiwa na Askofu Mkuu Desmond Tutu, ambayo, kwenye ripoti yake ya mwisho mwaka 2003, ilimlaumu kwa mabaya mengi yaliyotokea kwenye muongo mmoja uliopita wa utawala wa weupe.
|