|
Mwanamke ajinyonga kisa mumewe
2006-11-01 16:41:18
Na Waandishi Wetu, Jijini
Mwanamke mmoja mfanyabiashara amejinyonga kwa kutumia kipande cha khanga yake kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni mfarakano wa kifamilia kati yake na mumewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow amemtaja mwanamke huyo kuwa ni Aziza Jaffary, 30, mkazi wa Mabibo Loyola.
Amesema Bw. Rwambow kuwa mwanamke huyo amejinyonga chumbani kwake jana, akitumia kipande hicho cha khanga alichokuwa amekitundika kwenye kenchi la nyumba.
Kamanda Rwambow kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.
Wakati huohuo, moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme umeteketeza duka la kuuzia vinyago mali ya Bw. Ndele Mbwete, 45 huko Mwenge na kuteketeza kila kilichokuwamo ndani.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni Bw. Jamal Rwambow, amesema moto huo ulitokea jana saa 6:45 katika nyumba ya vyumba vitatu inayomilikiwa na Bw. Bruno Masakala iliyopo nyuma ya kituo cha kuuzia mafuta cha Bamaga.
Amesema thamani ya mali iliyoungua haijajulikana na moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto jijini kikishirikiana na wananchi.
|