01 Nov 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Majambazi yaua mfanyabiashara kwa risasi
 
2006-11-01 16:42:31
Na Romana Mallya, Ilala

Mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Kiasia wa Jijini Dar es Salaam ameuawa kinyama na majambazi. Majambazi hayo yasiyo na hata chembe moja ya utu, yamempiga risasi mdomoni zilizomfumua hadi kisogoni.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea juzi usiku na kumpotezea maisha mfanyabiashara Nurar Mansur Ally, 24, mmiliki wa sehemu ya mchezo wa kubahatisha iitwayo Nevada iliyopo katika mtaa wa Uhuru na Nyamwezi pale Kariakoo.

Hata hivyo, licha ya kuua, majambazi hayo hayakuambua chochote cha maana zaidi ya kukomba fuko la rambo yaliyodhani limejaa manoti wakati lilikuwana na funguo zaidi ya 15 za duka hilo, daftari kubwa la kuhifadhia kumbukumbu na mashine ya kufanyia mahesabu.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala Masindoki Masindoki.

Kamanda Masindoki amesema mauaji hayo yalitokea nje ya duka hilo wakati marehemu akitoka huku akiwa ameambatana na wafanyakazi wake wawili.

Amesema ghafla, marehemu alipigwa risasi iliyomlenga katikati ya pua na mdomo.

’’Baada ya kuanguka chini, majambazi hayo yalimpora mfuko huo wa rambo aliokuwa ameushikilia kisha yakatimua mbio na kujitoma kwenye gari yaliyokwenda nalo mawindoni,’’ akasema Kamanda Masindoki.

Amesema, majambazi hayo huku yakiamini yamepora mamilioni ya fedha zitokanazo na makusanyo ya mfanyabiashara huyo katika mashine zake kadhaa za mchezo wa kubahatisha, yaliyoyoma kama umeme.

Amesema mfanyabiashara huyo alikimbizwa hospitali ili kuokoa maisha yake lakini kwa bahati mbaya akafia njiani wakati akiwahishwa Muhimbili.

Amesema mwili wake umekabidhiwa kwa ndugu zake baada ya uchunguzi kufanyika.

Hadi sasa, amesema, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi mkali juu ya tukio hilo la kuhuzunisha.

Wakati huohuo, wanawake wawili wanaosadikika kuwa ni majambazi wanashikiliwa na polisi baada ya kuiba kompyuta ya mkononi (Laptop) pamoja na dola za Kimarekani 3,000.

Kamanda Masindoki amesema tukio hilo lilitokea katika hoteli ya Durban, Kariakoo Jijini Dar na akamtaja mmiliki wa mali iliyoibwa kuwa ni Bw. Salum Hamis Nassor, mkazi wa Zanzibar ambaye alikuwa mteja wa hoteli hiyo.

Amesema Bw. Nassor alipewa chumba namba B8 ghorofa ya tatu hotelini hapo.

Amesema pesa hizo zilikuwa kwenye komputa.
Amesema wakati mali yake inaibwa, yeye alikuwa eneo la chini ya ghorofa hiyo.

Amesema alibaini kwamba ameibiwa baada ya mhudumu wa hoteli hiyo, Bi. Anifa Hatibu, kumfuata na kumuuliza kama aliongozana na wanawake wawili.

Kamanda amesema alipomjibu kuwa hafahamu lolote kuhusu wanawake hao, mhudumu yule alimweleza kuwa chumba chake kimefunguliwa na baada ya kwenda chumbani kwake ndipo akabaini ameibiwa fedha pamoja na kompyuta.

Amesema baada ya polisi kufika hotelini hapo na kufanya upekuzi waliwakuta wanawake hao wakiwa kwenye chumba namba B4, wakiwa na kompyuta hiyo pamoja fedha hizo ambazo zilikuwa pungufu,dola 2300 badala ya zile zilizoibiwa dola 3000.

Ameongeza kuwa baada ya kuhojiwa wanawake hao walidai walifika hotelini hapo wakiwa wameambatana na mwanaume mmoja ambaye jina lake hawakulitaja wakiwa na funguo bandia na kufungua chumba hicho na kuiba.

Kamanda Masindoki amesema mwanaume huyo aliondoka na kiasi cha dola 700 pamoja na funguo hizo na kuongeza kuwa wanawake hao wamefikishwa mahakamani jana kujibu shtaka hilo la wizi.

Ameongeza kuwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kumsaka mwanaume aliyeshirikiana na wanawake hao katika wizi huo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.