21 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Pantoni Dar yajeruhi
 
2006-12-21 16:43:00
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili

Ubovu wa mlango mmojawapo wa pantoni ya MV Alina inayotumika kuvusha watu pale Kigamboni Jijini Dar, juzi ulimfanya abiria mmojawapo ajeruhiwe vibaya na kukimbiziwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa sasa akiwa hoi .

Abiria aliyekumbwa na balaa hilo na kujikuta akilazwa Muhimbili ni Mzee Omari Mmambira, 67, mkazi wa Ukonga Majumba Sita ambaye alikuwa akienda Kigamboni kuhudhuria kikao kimoja muhimu cha kuimarisha chama cha CCM ambacho yeye ni kiongozi mmojawapo katika Tawi la Ukonga Majumba Sita.

Akisimulia mkasa huo, Mzee Mmambira akasema tukio hilo lililomuacha hoi baada ya kubwagwa chini na kuvunjika mguu, limemtokea majira ya saa saa 6:00 hivi mchana upande wa Feri ya Magogoni wakati akiingia ndani ya pantoni hiyo kwenda Kigamboni.

Akasema, ilipofika muda huo, pantoni la MV Alina ambalo linalalamikiwa na wakazi wengi kutokana na ubovu, lilifika kwenye gati ya Magogoni na hapo utaratibu wa kushusha watu na magari ulianza na baadaye lilipokuwa leupe, ikafikia zamu ya kuchukua watu na magari na hapo ndipo purukushani ya kuingia kwenye pantoni ilipoanza.

Mzee Mmambira ambaye alikuwa mmoja wa abiria waliokuwa wakipigana vikumbo, hakuweza kutambua uozo wa mlango wa pantoni hiyo ambapo kuna sehemu inayoogopwa na watu wengi kutokana na kujaa utelezi.

Alipopiga hatua moja kuingia ndani, ndipo ghafla akajikuta akikumbana na utelezi huo mkali na papo hapo alianza kuyumba na kisha alianguka chini na kufikia juu ya sakafu ya gati.

’’Mimi si mtumiaji wa mara kwa mara wa pantoni, hivyo sikuwa ninafahamu hatari ya mlango ule mbovu.

Mimi nilipita sehemu hiyo na ndipo nilipoanguka ghafla na kunusurika kiajabu kutumbukia baharini...Mungu alikuwa upande wangu, vinginevyo, licha ya kuumia vibaya kama nilivyo sasa, ningeweza kufa kwa sababu kamwe nisingeweza kuogelea baada ya kuingia majini,’’ akasema Mzee Mmambira.

Akasema, baada ya kuanguka safari yake iliishia hapo kwani mguu wake ulivunjjika kabisa kabla wasamaria walioongozwa na wafanyakazi wa kituo hicho hawajamuwahisha hospitali.

Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa MOI Bw/ Almas Jumaa, Mzee huyo amefikishwa hapo akiwa hoi na mara moja akawahishwa wodini kabla ya kupatiwa matibabu zaidi.

Akasema, kwenye tukio hilo, mtu huyo amevunjika mguu wake wa kulia pamoja na kupata majeraha sehemu ya pajani na hatua muhimu ya kuunga sehemu iliyovunjika imeanza kuchukuliwa.

Mgonjwa huyo amelazwa wodi namba 17 jengo la Sewahaji na hali yake imeanza kuwa njema.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.