|
Kocha mpya wa Simba gumzo
2006-12-23 13:49:45
By Badru Kimwaga, Jijini
Wakati wenzao wa Yanga wakichekelea kupangiwa timu ya Visiwa vya Comoro wanayoamini ni vibonde, wanachama wa klabu ya soka ya Simba wamedai hawamjui vema kocha wao msaidizi mpya Madaraka Bendera.
Yanga itakayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa kuanza raundi ya awali na AGSM ya Comoro, wakati wenzao Simba watacheza Kombe la Shirikisho na Textile ya Msumbiji.
Baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga wamedai kuwa wanaimani kubwa kwa timu yao kusonga mbele katika raundi ya awali kwa timu waliyopangiwa nao ingawa hawaijui vema uwezo wao.
Aah Babu kama tukikwamia kwa Wacomoro basi haitakuwa na maana kwa timu yetu kushiriki michuano ya kimataifa, lakini tunaamini kabisa raundi ya kwanza tumetinga na hasa kwa vile tunaanzia nyumbani, Mohammed Ally mwanachama wa Yanga tawi la Magomeni Makuti alisema.
Alisema kuwa hata hivyo Yanga ina wajibu wa kujiandaa vema dhidi ya mchezo huo wa awali wa michuano ya klabu Bingwa Afrika pamoja na ile ya Kagame inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Wakati wanachama hao wa Yanga wakijinasibu hivyo, wenzao wa Simba wamedai wamepokea kwa mshtuko uteuzi wa kocha msaidizi mpya, Madaraka Bendera kwa madai hawamjui vema.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama wa Simba wamesema walitarajiwa kocha msaidizi angekuwa miongoni mwa makocha wenye majina waliokuwa wakitajwa kupewa nafasi hiyo kama Abdalla Kibadeni, Ally Bushiri ama Jamhuri Kihwelu.
Walisema kuwa hawaujui uwezo wa kocha wao mpya kwa vile hana jina kubwa, ila wanaamini viongozi wao wamefanya mambo kwa umakini.
Kwa kweli mimi simjui huyu kocha mpya, lakini kwa kuwa viongozi wetu tunawaamini basi ni lazima atakuwa ni kocha anayefaa na anaweza kuisaidia timu yetu, mmoja wa wanachama wa klabu hiyo Juma Ally (3453) alisema.
Mwanachama mwingine maarufu wa klabu hiyo (jina kapuni) alisema kuwa, watapima uwezo wa kocha huyo wakati wa kambi ya mazoezi inayoanza Jijini Desemba 28, na kipimo cha kwanza ni mashindano ya Mapinduzi Cup.
Hatuna haraka ya kuanza kupata wasiwasi na kocha huyo, kama viongozi wamemuona anafaa sisi tutampima kwa michuano ya Mapinduzi na katika kambi ya mazoezi ya timu yetu kwa michauno ya kimataifa, alisema.
|