|
Ekari 6,000 za pamba kufufuliwa Morogoro
2006-12-27 18:36:10
Na Aziz Issa
Kampuni ya Scott Enteprises inatarajiwa kulima mashamba mawili ya pamba mkoani Morogoro ambapo ekari zaidi ya 6,000 zitahusika katika mpango huo wa kufufua zao hilo.
Ofisa Mwendeshaji wa kampuni hiyo Bw. Kusanya Shindika, amesema kuwa shamba la kwanza lipo katika eneo la Duthumi ambapo linaukubwa wa eka 4,526.
Akasema shamba la pili ni lile lililopo katika eneo la Mkono wa Mara ambapo linajumuisha eka 1,500.
Akasema mashamba hayo awali yalikuwa chini ya chama cha wakulima Morogoro (MOFACU).
Kwa mujibu wa Bw. Shindika kampuni hiyo imeingia mkataba na MOFACU.
Pia kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika vijiji 27 katika msimu wa mwaka 2006/7.
Vijiji hivyo ni Kisaki, Gomero, Nyalutanga,Sesenga, Milengwelengwe, Muganzi, Vigolegole, Dakawa, Bonye, Mwade, Kirengezi, Mvuha,Kosonge.
Pia Dala, Kaganila,Pangawe, Mkono wa Mara, Mkambarani, BwakiraChini, BwakilaJuu. Kisanga Stendi,Selembara, Kingorwila na Ngerengere.
katika mpango huo wakulima wapatao 2875, wanatarajiwa kunufaika ambapo watalima eka 4,500.
Akasema watatoa mbegu za pamba kwa wakulima wa maeneo hayo na pia itaingia mkataba wa kusaidia upatikanaji wa pembejeo jirani na maeneo wanayoishi wakulima.
Aidha, akasema kampuni yake itashirikiana na wataalam wengine wa kilimo kama vile Chuo cha Utafiti Ilonga na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
Akawataka wakulima kuongeza ubora wa zao hilo na kuahidi kuwa kampuni itanunua zao hilo kwa wingi.
Akawataka kuondokana na hofu kwamba zao hilo litakosa soko.
|