|
Serikali ya Kata kujadili kujichanganya kwa DC Kndoni
2006-12-27 18:38:00
Na Abdul Mitumba, Makumbusho
Siku chache tu baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Fabian Massawe kutoa maamuzi yanayojichanganya kuhusiana na gesti moja inayoziba barabara pale katika Mtaa wa Minazini, uongozi wa Serikali ya Kata ya Makumbusho umeandaa Mkutano wa hadhara wenye lengo la kumthibitishia Mkuu wa wilaya hiyo kuwa kachemsha kwa kuitetea gesti hiyo ili iendelee kuwakera wananchi walio wengi.
Hivi karibuni, Bw. Massawe alikaririwa akitoa agizo la kutaka gesti hiyo yenye kuzua mgogoro mtaani ibomolewe.
Lakini siku chache baadaye, bosi huyo wa wilaya akaonekana kama amejichanganya kwa kukiri kuwa alikosea na kubatilisha maamuzi yake ya awali yaliyotaka gesti hiyo isiendelee kuwepo na badala yake kutaka iachwe kama ilivyo.
Lakini sasa, Serikali ya Kata ya Makumbusho imeamua kuitisha Mkutano huo wa hadhara, ikisema kuwa lengo ni kumthibitishia Mkuu wa Wilaya yao kuwa mfanyabiashara mwenye gesti hiyo iliyojengwa katika eneo linaloziba mtaa, ameshalipwa chakesiku nyingi na hivyo kinachotakiwa sasa, ni kuibomoa na kuwaondolea kero wananchi wa mtaani hapo.
Diwani wa kata ya Makumbusho, Bw.Christopher Mutayoba, amesema juzi kuwa mkutano huo ndio utakaotoa ushahidi wa mwisho juu ya uhalali wa mmiliki huyo kuendelea kubaki hapo au kubomoa nyumba yake.
Hata hivyo, Bw.Mutayoba alisema mkutano huo hauna maana unapingana na kauli ya mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, ambaye hivi karibuni alisema mwenye nyumba hiyo, Bw.Elikunda Malewo, ana haki ya kuendelea kubaki mahala hapo.
Kuna mambo yamejificha juu ya suala hili. Lakini sisi, kama watendaji wa kata, hatutaki kuwasemea wananchi.
Badala yake tumeandaa mkutano wa hadhara na watu walioishi katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa miaka ya 70 watatoboa siri ya kile wanachokijua kuhusu eneo hilo, akasema Diwani Mutayoba.
Akaeleza zaidi Mutayoba kuwa mmiliki wa gesti hiyo, amekuwa akitembea na ramani inayoonyesha eneo hilo siyo barabara, lakini ukweli ni kwamba yapo madai ya kuthibitisha kuwa ramani hiyo imetengenezwa kiujanja hivi karibuni ili kuhalalisha uwepo wa gesti hiyo inayoziba mtaa.
Kauli ya diwani Mutayoba inafuatia hivi karibuni DC Massawe kutangaza kufuta agizo alilotoa awali la kumtaka mmiliki huyo kuvunja nyumba yake ndani ya siku saba tangu alipofanya ziara ya kukagua usafi na matumizi ya ardhi katika kata ya Makumbusho.
Alitoa agizo hilo baada ya viongozi wa kata hiyo, akiwemo diwani Mutayoba kumwambia kuwa Bw.Malewo alishalipwa fidia muda mrefu lakini amegoma kuvunja nyumba yake, hivyo kuendelea kuziba mtaa huo na magari kushindwa kupita.
Katika ufafanuzi wake wa awali, DC Massawe alisema mmiliki wa nyumba hiyo alipata hati halali ya kumiliki kiwanja hicho Na.719 ya mwaka 1978 na baadaye hati ya kumiliki nyumba Na.D/KN/A/12330.
|