27 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watatu Jijini wafa kilele cha ’Boxing Day’
 
2006-12-27 18:39:26
Na Mwanaidi Swedi, Jijini

Katika hali ya kuhuzunisha, watu watatu wamefariki dunia Jijini Dar jana katika siku maalum ya kupeana zawadi baada ya ile ya sikukuu ya Krismas juzi (Boxing Day).

Watu hao wamekufa kutokana na matukio tofauti ya ajali za barabarani na mmoja anayedaiwa kujinyonga hadi kufa.

Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Bw. Jamal Rwambo, amesema katika tukio la kwanzapale katika maeneo ya Goigi Mbezi Beach, mtu aliyefahamika kwa jina la Juma Tefano ama Jay Mo, mkazi wa Mbezi Juu, amejikuta akipoteza maisha baada ya kugongwa na gari na kufa.

Kamanda Rwambo amesema kuwa tukio hilo limetokea jana, mishale ya saa 7:45 mchana wakati marehemu akijaribu kuvuka barabara na kugongwa na lori aina ya Isuzu Tipper, lenye namba za usajili T576 AHA.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti Muhimbili na dereva wa gari hilo bado anasakwa.

Katika tukio jingine lililojiri pale katika barabara ya Uhuru, maeneo ya Rozana, kijana mmoja wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 na 25, amekutwa amekufa baada ya kugongwa na gari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Masindoki Masindoki, amesema tukio hilo limejiri majira ya saa 1:30 usiku jana ambapo mtu huyo aligongwa na kufariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Amana.

Gari lililomgonga mtu huyo ni daladala aina ya Isuzu Journey, lenye namba T634 AEK, likifanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Tabata Jijini Dar.

Dereva wa gari hilo bado anasakwa na polisi wakati mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa pale katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika tukio la tatu, Mkazi wa Kigamboni Mji Mwema, Bw. Bernad Poul, 54, ambaye kazi yake ni kugonga kokoto, amekutwa amejinyonga na kamba ya katani aliyokuwa ameitundika kwenye kenchi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Bw. Kandihabi, amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 11:00 jioni huko Kigamboni.

Amesema Kamanda Kandihabi kuwa kabla ya kujinyonga, marehemu alikuwa akisumbuliwa muda mrefu na maradhi ya kifua.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.