|
Maiti yenye cocaine
2006-12-27 18:40:40
Na Job Ndomba, Jijini
Siku chache tu baada ya kunaswa kwa maiti yenye shehena ya ujazo wa kilo moja ya madawa ya kulevya aina ya Cocaine pale Jijini Mbeya, Jeshi la Polisi nchini limeunda kikosi maalum cha kuwasaka waliohusika kwa njia moja ama nyingine na dili hiyo.
Kamanda wa Jeshi hilo Jijini Mbeya, Suleiman Kova, ameiambia Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi kuwa sasa, kama ilivyo kwa majambazi na wahalifu wengine, wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kamwe hawatapumua Jijini kwake.
Tulipata habari za tukio hili saa 24 kabla... tukaunda kikosi maalum (Task Force) na kwa hakika, kazi ya kunasa wale waliohusika kwa njia moja ama nyingine na dili hii inaendelea vizuri, akasema.
Amesema wanashirikiana na kikosi maalum cha udhibiti wa dawa za kulevya nchini na pia polisi wa Zambia.
Tutahakikisha mtandao wa watu hawa unasambaratika mara moja kwa sababu tumepania kivitendo kutekeleza azma hiyo, akasema Kamanda Kova.
Kauli hiyo imekuja wakati kuna taarifa kuwa baadhi ya vigogo wanaohusika na biashara ya unga hapa Jijini, presha imewapanda kutokana na hofu ya kuhusishwa na dili hiyo ya kusafirisha madawa ndani ya maiti.
Wakati huohuo, imebainika kuwa baada ya tukio hilo la Jijini Mbeya, baadhi ya vigogo wa biashara ya dawa hizo Jijini Dar wamejawa na kihoro, wakihofu kuwa sasa mambo yamewaharibikia na siku zao za kukamatwa zinahesabika.
Kitendo cha Kamanda Kova na askari wenzie Jijini Mbeya kustukia chezo la usafirishaji wa maiti hiyo yenye shehena ya Cocaine, huku wakiwabana wahusika na kuwataja vinara wao mmoja baada ya mwingine, kinadaiwa kuwapandisha BP vigogo wa biashara hiyo Dar.
Hivi sasa, inadaiwa kuwa baadhi yao ambao hutamba kwenye mikoko ya bei mbaya, hawana raha na nyendo zao zimeanza kubadilika.
Katika tukio hilo, mwili wa kijana mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Kombo Abdallah wa Tanga, ilikutwa ikiwa imewekwa kilo moja ya madawa aina ya Cocaine.
Madawa hayo yaliyokuwa yamewekwa tumboni, yanatajwa kuwa na thamani ya Sh. Milioni 26.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, tayari kikosi chake maalum kimeshawatia mbaroni watuhumiwa kadhaa, akiwemo mfanyabiashara mmoja maarufu aitwaye Hamza Hassan Lema, 34, anayedaiwa kudili na biashara hiyo ya unga licha ya kumiliki duka kubwa la vifaa vya umeme huko Tunduma.
Wengine waliotiwa mbaroni mpaka sasa kuhusiana na tukio hilo ni Hemed Juma, 34, , 29, Andrew Mwakikato, 26, Hamis Nangash, 28, Jushua Charles, 29, Amor Salum, 30, Edward Maiko, 28 na Omary Hussein.
Watuhumiwa hao walikamatwa kwa mara ya kwanza katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi, kilomita 30 kutoka katika mpaka wa Zambia na Tanzania, wakiwa wanasafirisha maiti iliyosheheni madawa hayo ya Cocaine kuelekea mkoani Tanga.
|