|
Jamaa afoji saini ya JK
2006-12-27 18:41:38
Na Idda Mushi, PST - Morogoro
Mtu mmoja ametoa kali ya kufungia mwaka kwa kujaribu kuuiga mwandiko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bwana Jakaya Kikwete na kisha kujiandikia barua kwenda ofisi moja nyeti akitaka apewe kazi kwa kimemo cha Rais.
Jamaa huyo alitaka kazi katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mjini hapa.
Mtu huyo ametajwa kwa jina la Aloyce Sotel, 48, mkazi wa Bongola pale Kilakala mjini Morogoro.
Imeelezwa kuwa aliiga mwandiko wa Rais Kikwete, akaandika barua ya kuamuru uongozi wa Chuo hicho kumpa kazi na kisha akaangusha saini ya mkuu huyo wa nchi na kugonga muhuri wa ikulu kabla hajastukiwa na kudakwa.
Hata hivyo, fiksi hizo za aina yake zimemuweka pabaya Bw. Sotel.
Amejikuta akipewa kifungo cha miaka saba jela baada ya hivi juzi, Mahakama ya Mkoa huu kumtia hatiani.
Akitoa hukumu kwa Sotel, Hakimu Mkazi Bw. Wilbard Bampikya, ameelezea kuridhishwa kwake na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kutoa adhabu hiyo ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kughushi nembo kwa ajili ya kufanikisha mambo yao mbalimbali kinyume cha sheria.
Awali, Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi Ali Wendo, alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Juni 10 mwaka huu.
Akasema Mwendesha Mashitaka huyo kuwa mshtakiwa alikwenda chuoni SUA na kutoa maagizo feki kwa aliyekuwa Kaimu Mkuu wa chuo, Bw. Gerald Monera, ya kumtaka ampe kazi Sotel katika Idara ya Misitu.
Akasema Mwendesha Mashtaka kuwa maagizo hayo ambayo mshitakiwa aliyawasilisha kwa barua, alidai yametoka kwa Rais mwenyewe wakati ukweli ni kwamba ni yeye ndiye aliyeandika barua hiyo na kufoji nembo na muhuri wa Ikulu.
Akasema Mwendesha Mashtaka kuwa kabla ya Bw. Sotel kukamatwa, Kaimu Mkuu huyo wa Chuo alistukia uongo wa mshitakiwa baada ya kuona mwandiko uliotumika katika barua hiyo umetofautiana na ule wa Rais Kikwete ambao anaufahamu.
Baada ya hapo, ikadaiwa kuwa Mkuu wa Chuo aliwataarifu watu wa Usalama wa Taifa mkoani hapa ambao nao walifika na Polisi na kumkamata mshitakiwa.
Ikaelezwa zaidi kuwa mshitakiwa alipobanwa kwa maswali, akakiri kufanya kosa hilo na akajitetea kwamba alifanya hivyo ili apate ajira kwa urahisi.
Baadaye, ikaelezwa kuwa Polisi waliamua kwenda nyumbani kwa mshitakiwa na kufanikiwa kupata vyeti mbalimbali vikiwa na majina ya Juma Sotel na Aloyce Sotel.
Lakini katika utetezi wake kortini, mshitakiwa Sotel alianza kwa kukana kuhusika na kughushi huko, akidai kuwa aliyetenda kosa hilo ni pacha mwenzie na kwamba yeye aliwakubalia polisi ili kujiepusha na kipigo kikali toka kwao.
Hata hivyo, akadai katika utetezi wake uliokosa nguvu kortini kuwa yeye hajawahi kufika chuoni SUA na kwamba pacha wake aliyezua soo hilo, ameingia mitini na hadi sasa hajui aliko.
|