|
Washirikina CCM wasipewe nafasi-Mbunge
2006-12-28 16:22:44
Na Sabato Kasika, Jijini
Wakati Chama cha Mapinduzi,CCM, kiko mbioni kufanya uchaguzi wa viongozi wake wa ngazi mbalimbali, wanachama wa chama hicho tawala wametakiwa kuwapiga chini wale wote wanaotaka kuongoza wakitumia nguvu za waganga wa kienyeji kupata nafasi hizo.
Chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi huo mwakani ambapo wanachama na viongozi wa ngazi mbambali mkoani Dar es Salaam, wamekuwa wakipewa semina za jinsi ya kuandaa na kufanikisha uchaguzi.
Akizungumza kwenye mkutano wa kumsimika mlezi wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata ya Manzese, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Dar es Salaam ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Azzan Zungu, amesema baadhi ya wanachama wamekuwa na tabia ya kusaka vyeo kwa nguvu za giza.
Mwenyekiti huyo alimsimika Bw. Johanes Mbuge na kusema umefika wakati sasa wa kuchagua viongozi wenye nia ya kukitetea chama na serikali na siyo wale wanaosaka vyeo kwa waganga bila kujua kwamba vyeo anatoa Mungu.
Mungu ndiye anaweka serikali madarakani na ndiye anayechagua viongozi, wale wanaokwenda kwa waganga hawafai kuwa viongozi...wale ambao watabainika wanapeleka ngombe, mbuzi na kuku kwa waganga ili wapate vyeo hawatufai, wakataeni, akasema Bw. Zungu.
Naye Mlezi wa Jumuiya hiyo Kata ya Manzese, Bw, Mbuge, baada ya kusimikwa, aliahidi kutoa Sh. Milioni Moja ambazo zitasaidia kukarabati ofisi ya Jumuiya hiyo na pia kuweka vifaa vya kiofisi ili ionekane ya kisasa zaidi.
Mbali na hilo, mlezi hiyo aliahidi kushirikiana na viongozi wa Jumuiya na chama katika kusaidia kwa kila hali na mali kushawishi vijana ambao wako eneo la Uwanja wa Fisi kuachana na tabia chafu ikiwemo ya ukahaba na utumiaji wa dawa za kulevya ili nao wajiunge kwenye jamii na kufanya shughuli za maendeleo.
|