|
Risasi zarindima
2006-12-28 16:23:14
Na Waandishi Wetu
Kama ungetembelea kijiji cha Uyovu, kilichoko Wilaya ya Bukombe mkoani Shinyanga majuzi, ungedhani umefika eneo la mapambano kutokana na risasi zilizokuwa zikirindima.
Imeelezwa kuwa katika tukio hilo watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walitolewa roho papo hapo.
Marehemu hao inadaiwa walizidiwa akili na wenzao wakati wakiwa kwenye mgao wa mali ya machumo\ yaani mapesa waliyokomba.
Habari zaidi zinasema wahusika katika tukio hilo baadhi ni raia wa nchi jirani ya Burundi ambao ndio inasemekana walihusika na mauaji hayo.
Hata hivyo taarifa za kipolisi zinasema tayari watuhumiwa hao wametiwa mbaroni.
Imeelezwa kuwa walikutwa wakiwa na bunduki hatari aina ya FN.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga, Sirro Nyankoro amethibitisha tukio hilo.
Amewataja majambazi waliokamatwa kuwa ni Petro Edward, 29, George Seleman, 31, wakazi wa kijiji cha Uyovu, Gerald Mbiho,34 na Lonjino Bernado,33, wote raia wa Burundi, wanaoishi katika kijiji cha Uyovu wilayani humo.
Aidha, Kamanda Nyankoro aliwataja majambazi yaliyouawa na wenzao kuwa ni Boniface Shitta, 23 na Majaliwa Balagoma, 27 ambao nao ni wakazi wa kijiji cha Uyovu.
Amesema watu hao wamedhulumiana kiasi cha Shilingi milioni 1.5, walizokuwa wamepora hivi karibuni katika shughuli yao ya ujambazi.
Na huko Zanzibar, majambazi yenye silaha, yamepora zaidi ya Sh milioni 9.5 katika kituo cha afya.
Imeritiwa kuwa majambazi hayo yalimevamia Hospitali ya Kituo cha Afya cha kutibu ugonjwa wa kichocho kilichopo eneo la Lumumba, Zanzibar na kupora Sh. milioni 9.5.
Mkurugenzi wa Afya Jamii Zanzibar, Bw Juma Rajab, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Bw. Juma amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi, ambapo majambazi hayo yaliezua sehemu ya paa la jengo hilo na kujitoma ndani kabla ya kupora fedha hizo.
|