04 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vijiji vyapewa mabuti ili kusimamia maliasili zao
 
2007-01-04 17:45:43
Na Job Ndomba, Jijini

Vijiji kadhaa wilayani Rufiji na mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi, vimepata viatu aina ya buti kwa ajili ya kuvitumia wakati wakiwa kwenye harakati za kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.

Mbali na mabuti hayo yaliyokuwa zaidi ya 50, Serikali imeshauriwa kutumia mamlaka za misitu kuwaelimisha wananchi kuhusu sera na sheria zinazohusu usimamizi shirikishi wa misitu.
Imeelezwa kuwa uzoefu umeonesha wananchi wengi hawazijui sheria hizo wala miongozo yake.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mtaalam wa Misitu ambaye pia ni Meneja Uendeshaji wa Mradi wa Kuhifadhi mti aina ya Mpingo,MCP, Bw.Gasper Makala wakati akitoa msaada wa vitendea kazi kwa Kamati za Vijiji za usimamizi wa misitu.

Bw.Makala amesema sera na sheria nyingi zikitungwa huishia kufungiwa kwenye makabati huku wananchi wakishindwa kufahamu hata sheria ndogo zinazolinda rasilimali zao.

“Sheria nyingi zipo ofisini, hata zile zinazosimamia sera za misitu hazijulikani kwa wananchi na hivyo kuwafanya washindwe kuzifahamu.

“Ni muhimu wananchi wakafahamu maana halisi ya usimamizi shirikishi wa misitu na kuweza kujipatia faida zitokanazo na rasilimali hiyo,” akasema Bw.Makala.

Mradi wa MCP umetoa viatu aina ya mabuti (gumboots) jozi hamsini zenye thamani ya shilingi 500,000 kwa kamati za vijiji ili kutunza na kusimamia maliasili za Kata ya Kikole Wilayani Kilwa.

Amevitaja vijiji vilivyofaidika na msaada huo kuwa ni Kikole, Migeregere, Ruhatwe na Kisangi vyote vya Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Bw. Makala amesema lengo la msaada huo ni kuboresha utendaji kazi wa wajumbe wa kamati za Maliasili vijijini ili kuwanusuru na athari wanazoweza kukumbana nazo wakati wanaposimamia rasilimali hiyo.

Bw.Makala amesema mradi huo umeamua kutoa msaada huo kwa kutambua mahitaji muhimu ya jamii katika shughuli za usimamizi shirikishi wa misitu.

Naye Diwani wa Kata ya Kikole aliyekabidhiwa msaada huo kwa niaba ya Kamati hizo Bw,Haji Mulike amesema kuwa msaada huo ni changamoto kubwa kwa watu wake katika kuhakikisha wanatunza na kusimamia vizuri misitu.

Bw. Mulike amesema atahakikisha wananchi hao wanautumia msaada huo vizuri ili kuheshimu mchango wa asasi hiyo katika kutoa huduma kwa jamii.

MCP ni Asasi isiyo ya kiserikali iliyopo katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi inayojishughulisha na masuala ya uhifadhi wa Misitu kwa kutekeleza mpango wa kitaifa wa Usimamizi shirikishi wa Misitu kwa kushirikiana na Wilaya hiyo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.