|
Radi yaua mtu Kibaha
2007-01-04 17:48:19
Na Janneth Kiure, Kibaha
Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimeua mtu mmoja papo hapo na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi huko katika Kata ya Kwalla wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati wakitembea barabarani.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw. Shaibu Ibrahim, amesema kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya saa 1:00 jioni ambapo walipigwa na radi iliyosababishwa na mvua kubwa na upepo mkali.
“Wananchi wanapaswa kuwa makini wakati wa mvua za vuli ikiwa ni kuzuia watoto wasiende kucheza ovyo kwenye madimbwi ili kuepuka majanga kama hayo,” amesema Kaimu Kamanda huyo.
Akamtaja aliyekufa papo hapo kuwa ni Msafiri Msafiri, 45 na majeruhi ni Sauda Juma, 30, wote wakazi wa Dutumi Kata ya Kwalla.
Baadhi ya wakazi wanaoishi katika kijiji hicho wamesema kuwa mvua hizo zinazonyesha Mkoani Pwani, zimeleta hasara kubwa kutokana na mashamba yao kufunikwa na maji pamoja na bara bara kukatika na kusababisha usumbufu mkubwa ambapo mito mingi imejaa ghafla.
Wakasema kuwa mvua hizo endapo zitaendelea kunyesha huenda zikaleta madhara makubwa kwa wananchi na kusababisha janga kubwa la njaa kwani mazao mengi yamefunikwa na maji mengi lakini tunamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani DC Christine Ishengoma, kwa juhudi zake za kutembelea maeneo kadhaa yaliyopatwa na mafuriko.
“Mvua hizo zimeleta matatizo makubwa ambapo wengine wameshindwa hata kwenda mashambani mwao. Pia kuna hatari nyumba zilizojengwa kwa miti zikabomoka katika kipindi hiki,” akasema mwananchi huyo.
|