04 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waziri Akukweti afariki dunia
 
2007-01-04 17:52:09
Na Waandishi Wetu, Jijini

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Bwana Juma Akukweti, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nchini Afrika Kusini alikopelekwa na Serikali kwa ajili ya matibabu.

Alifia katika hospitali ya Milpark iliyopo Jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini alikohamishiwa mnamo Desemba 27 mwaka jana, akitokea katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

Taarifa kutoka kwa chanzo chetu huko Afrika ya Kusini zinasema Waziri Akukweti alifariki majira ya saa nane usiku, ikiwa ni siku ya 20 tangu alipopata ajali ya ndege huko mkoani Mbeya.

Ingawa Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na kifo cha Waziri huyo, lakini baadhi ya maafisa wake wa juu wamethibitisha kuwa Waziri Akukweti amefariki jana usiku.

``Ni kweli Waziri Akukweti amefariki, ila taarifa rasmi zitatolewa baadaye,`` amesema afisa mmoja wa Serikali.

Kifo hicho kinafanya idadi ya abiria waliofariki katika ajali ya ndege iliyoanguka mjini Mbeya mwezi uliopita
Kuwa wanne kati ya sita waliokuwemo.

Katika ajali hiyo, Waziri Akukweti alijeruhiwe vibaya sehemu mbalimbali mwilini.

Awali, kulikuwa na taarifa za matumaini juu ya afya yake ambapo ilielezwa kuwa mwishoni mwa Desemba, alifanyiwa upasuaji wa kwanza kwenyemguu wake wa kushoto. Kisha ikaelezwa kuwa amefanyiwa upasuaji mwingine kwenye mguu wa kulia.

Taarifa zilisema miguu yote ya marehemu ilikuwa imeungua vibaya kwa moto ulioibuka baada ya ndege kudondoka.

Baadaye, taarifa toka kwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Emmanuel Mwambulukutu, zilisema kuwa Waziri Akukweti angefanyiwa upasuaji mwingine mapema wiki hii kwenye mguu wake wa kushoto na kupandikiza ngozi mpya eneo ambalo limeathirika zaidi kwa moto.

Pia ilielezwa kuwa baada ya upasuaji huo wa mguu wa kushoto kufanyika, ungefuata upasuaji mwingine kesho.

Waziri Akukweti na watu wengine watano walianguka na ndege ya kampuni binafsi ya Tanzanair, aina ya Cessna 310, yenye namba za usajili 5H-TZ . Ajali hiyo ilitokea mishale ya saa 12:55 asubuhi baada ya ndege hiyo kuruka umbali wa mita 200 kutoka kwenye Uwanja wa Ndege Mbeya.

Katika ajali hiyo mpigapicha wa Idara ya Habari, MAELEZO, Bi. Theresia Nyantori alifariki dunia papo hapo. Abiria wengine walifariki baada ya kufikishwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Waliopoteza maisha yao ni pamoja na Mratibu Mkuu wa Mpango wa Uendelezaji Masoko ya Mazao ya Kilimo, Bw. Nathael Katimila na Bw. George Bendera.

Akukweti ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru mkoani Ruvuma tangu mwaka 1990, alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1947.

Amewahi kutumikia Serikali katika nafasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa.

Akukweti ana Stashahada ya Uongozi wa Jamii aliyoipata katika Chuo cha Esami mkoani Arusha na pia Shahada ya Elimu aliyoipata mwaka 1975.

Masomo ya awali aliyapata katika shule za Msingi Mataka na Ligoma kabla ya kujiunga na shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (1966 hadi 1970) na kisha akaendelea na elimu ya juu ya Sekondari Tabora kuanzia mwaka 1970 hadi 1971.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.