|
Diwani alia na wavuvi wanaoangamiza mikoko Mbweni
2007-04-20 16:27:35
Na Fransisca Jeremiah, Mbweni
Diwani wa kata ya Mbweni iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar, Bw. Hashim Mbonde, amesema atawachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara na wavuvi wote wa samaki waliopo pembezoni mwa fukwe za bahari katika eneo hilo endapo hawataacha tabia ya kuchafua mazingira.
Bw. Mbonde amesema wafanyabiashara na wavuvi wengi waliojianzishia kambi katika eneo hilo wamekuwa na tabia ya kuharibu mazingira kwa kukata miti ya mikoko hovyo na pia kujisaidia katika vichaka vya miti hiyo.
`Hali hiyo ni ya hatari. Badala ya kuyatunza mazingira, wao wamekuwa wachafuzi kwa kwenda kujisaidia hovyo vichakani na kuhatarisha afya za watu, ` akasema diwani huyo.
Bw. Mbonde amesema wavuvi hao wanaoendesha shughuli zao na kuishi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo lao, wamekuwa pia mstari wa mbele katika kuvua samaki wadogo.
Akasema wavuvi hao wako katika vikundi vikundi na uwingi wao pia ni hatari kwa fukwe hizo.
Akasema baadhi ya wavuvi hao hawana uchungu na mazingira hayo kwa vile wanatoka katika maeneo ya mbali na wengine hutoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na Malawi, Uganda, Msumbiji na kwingineko.
“Wanakata mikoko kama hawana akili nzuri… sisi hatuwezi kulivumilia jambo hilo na kama hawajirekebishi, tutawachukulia hatua za kisheria,” akasema Bw. Mbonde ambaye pia amesema wako mbioni kuliomba Jeshi la Polisi kwenda kuongeza doria huko ili pia kupunguza vitendo vya kihalifu.
|