|
Mapesa ya JK: Kaa chonjo, watu kibao wameibiwa
2007-04-20 16:30:25
Na Amri Lugungulo, PST - Rufiji
Kama na wewe uko kwenye mchakato wa kufuatilia mapesa yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya wajasiriamali nchini, almaarufu kama Mabilioni ya JK, ni vyema ukakaa chonjo kwani usipofanya hivyo, unaweza kujikuta ukiibiwa huku ukijiona.
Tahadhari ya aina hiyo kuhusiana na `Mapesa ya JK` inatokana na ukweli kuwa hadi sasa, watu kibao wameshalizwa senti zao baada ya kufuatilia mikopo hiyo kichwa-kichwa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Alasiri imezinyaka toka maeneo mbalimbali ikiwemo Rufiji mkopani Pwani, ni kwamba baadhi ya wananchi hivi sasa wako kwenye msiba mzito baada ya kuliwa senti zao na wajanja waliojifanya ni maafisa wa benki wanaokusanya fedha kwa watu ili wawasaidie kulamba kiulaini mabilioni hayo ya JK.
Waliopigwa changa la macho hivi karibuni ni wajasiriamali kibao wa kijiji cha Nyamisati, kata ya Salali, wilayani Rufiji.
Watu hao inaelezwa walijifanya watumishi wa benki ya NMB na wakawataka wakate dau la shilingi 2,000 kila mmoja ili waandaliwe michanganuo ya biashara ya kwenda kuombea mikopo.
Taarifa ya kutapeliwa ilifichuliwa na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanywa na baadhi ya Wenyeviti wa UWT toka wilaya mbalimbali za mkoa wa Pwani.
Katika mkutano huo, kiongozi mmoja wa kijiji aliwaambia wenyeviti hao kuwa wakati wanatapeliwa waliambiwa pesa hizo ni kwa ajili ya malipo ya kutengenezewa michanganuo ya biashara ya kwenda kuombea mikopo.
Akasema kwa vile wao hawafahamu kutengeneza hiyo michanganuo ya biashara, waliingia laini na kuwapa pesa watu hao waliojifanya ni watumishi wa benki.
Akasema ingawa wajasiriamali wengi katika kijiji chao ni maskini wa vipato, lakini walijitahidi kadri wanavyoweza katika kuchanga Sh. 2,000 kila mmoja ili kupata mikopo hiyo na hatimaye kujikwamua kimaisha kupitia biashara.
Lakini, kiongozi huyo akasema kuwa walichokuja kuambulia ni kilio baada ya michanganuo hiyo ya kibiashara kutupiliwa mbali na benki kwa kuonekana kuwa imeandaliwa ovyo.
“Tulishatoa pesa zetu tukitegemea kuwa tutafanikiwa kupata mikopo hii… kumbe mambo yamekuwa tofauti, wengi tumerudishiwa mikaratasi yetu tukiambiwa tumeandika ovyo, imetushangaza na kwakweli inauma sana, “ akasema mmoja wa wanawake waliodai kutapeliwa na watu hao waliojitangaza kuwa ni watumishi wa NMB.
Hata hivyo, baada ya kutoa kilio chao, kiongozi mmoja wa kijiji alisimama na kuwalaumu watu hao, hasa akinamama ambao walikubali kuliwa pesa zao na kuwaambia kuwa walipaswa kwenda kuwaona maafisa wa biashara, maafisa wa maendeleo ya jamii na wa maafisa wa ushirika.
Akawaambia kuwa maafisa wanaotambulika na Serikali, ndio ambao tuyari wamefundishwa namna ya kuwasaidia kupata mikopo hiyo na wala si vinginevyo.
Haikujulikana katika mkutano huo kuwa ni mapesa kiasi gani yametapeliwa kwa wananchi, ingawa ilibainika kuwa waliotozwa Sh. 2,000 kila mmoja walikuwa wengi mno.
|