|
Majambazi hoi: Moja lapigwa risasi, jingine lanaswa porini
2007-04-20 16:31:21
Na Elisante John, PST-Singida
Jeshi la Polisi nchini limeendelea kuwabana pabaya majambazi ambapo hivi karibuni, limeweza kuwanasa watu wawili wanaotajwa kuwa ni miongoni mwa majambazi hatari zaidi.
Kwa nyakati tofauti, jeshi hilo limelikurupusha jambazi moja lililokuwa kwenye maficho yake ya muda mrefu msituni na pia, limeweza kumlamba risasi mbili za paja mtu mwingine wa aina hiyo aliyekuwa akijaribu kutoroka chini ya ulinzi mkali wa gereza.
Taarifa za jeshi hilo zinasema, mmoja wa majambazi hatari zaidi amenaswa katika msitu wa Lugoba pale Chalinze mkoani Pwani.
Mtu huyo hatari, ametajwa kwa jina la Msafiri Changale a.k.a Morimori, mkazi asiye na maskani maalum mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bw. Shaibu Ibrahim, amesema jeshi lake limemnasa mtu huyo hatari kufuatia msako kabambe ulioendeshwa hivi karibuni.
Akasema mtuhumiwa huyo hatari, alidakwa katika msitu wa Lugoba pale Chalinze mkoani humo, ambako alikuwa amejificha katika moja ya ngome zake muhimu.
“Mtuhumiwa huyu amekuwa akisakwa kwa muda mrefu… nadhani ni hatua nzuri katika vita hii ya kila siku dhidi ya vitendo vya kihalifu,” amesema Kamanda Ibrahim, bila kufafanua zaidi.
Wakati huohuo, Jeshi hilo limeweza kumtia mbaroni kijana mmoja anayedaiwa kuwa hatari zaidi katika uporaji wa kutumia silaha mjini Iramba mkoani Singida.
Mtuhumiwa huyo, sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba baada ya kupigwa risasi mbili za paja lake la kushoto baada ya jaribio lake la kutoroka toka kwenye ngome ya jela kugonga mwamba.
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Celina Kaluba, amesema kuwa tukio hilo limetokea hivi karibuni katika eneo la Kiomboi wakati mshitakiwa huyo na wenzake 26 wanaokabiliwa na makosa mbalimbali wakiingizwa kwenye gereza la Kiomboi wilayani humo.
Mtuhumiwa huyo hatari, ametajwa kwa jina la Ntandu Athumani, 25, mkazi wa kijiji cha Iguguno wilayani Iramba.
Akisimulia kisa hicho, Kamanda Kaluba akasema majeruhi huyo akiwa na wenzake 26 ambao walikuwa wakisindikizwa na askari watano kwa ajili ya kuingizwa mahabusu, alichomoka ghafla toka kundini na kuanza kutimua mbio wakati wakiwa tayari kwa kuingizwa gerezani.
Hata hivyo, akasema Kamanda Kaluba kuwa mshtakiwa huyo alifanikiwa kukimbia umbali wa mita 30 tu kutoka gerezani kabla ya kupigwa risasi mguuni na askari D. 3806 CPL Robert aliyekuwa umbali wa mita ishirini kutoka kwa mtuhumiwa.
Akasema kabla ya hapo, askari alishapiga risasi tatu hewani ili kumtisha mahabusu huyo lakini hakutishika na badala yake akaendelea kukimbia kabla ya kujikuta akigaagaa chini baada ya risasi mbili kumpata kwenye paja.
Kamanda Kaluba amesema mshitakiwa anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha , yenye jalada namba KIO/118/2007 CC.NO.15/2007.
Akaongeza Kamanda Kaluba kuwa atakapopata nafuu, mtuhumiwa huyo wa uporaji atafikishwa mahakamani ili pamoja na kosa lake la mwazo pia kukabiliana na kosa jipya la kujaribu kutoroka gerezani.
|